Nadia Mukami na Arrow Bwoy wafichua kwa muda gani walikuwa wameachana, kwa nini

Arrow Bwoy alidokeza kuwa kiburi kati yao kiliwafanya wasikae chini na kutatua mzozo wao.

Muhtasari

•Katika mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni, wawili hao walieleza kwamba walienda njia tofauti kufuatia mzozo wa kinyumbani.

"Baada ya kujifungua na najaribu kujiinua. Ilikuwa ngumu kwangu. Nilipitia msongo wa mawazo baada ya kujifungua," Nadia alisema.

Nadia Mukami na Arrow Bwoy
Image: HISANI

Wanandoa mashuhuri Nadia Mukami na Arrow Bwoy wamefichua kwamba walitengana kwa kipindi cha takriban wiki mbili mwaka jana.

Katika mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni, wawili hao walieleza kwamba walienda njia tofauti kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Nadia alifichua kwamba mumewe aliondoka nyumbani baada ya wao kuzozana.

"Niliondokea pressure kidogo. Unajua ukiwa na mwenzako alafu uone mambo imeenda mrama, wakati mwingine ni vizuri kujipatia nafasi," Arrow Bwoy alijitetea.

Alidokeza kuwa kiburi kati yao kiliwafanya wasikae chini na kutatua mzozo wao.

Nadia alikiri kwamba alizidiwa na mambo mengi ambayo yaliyomkumba baada ya kujifungua mapema mwaka jana.

"Baada ya kujifungua na najaribu kujiinua. Ilikuwa ngumu kwangu. Nilipitia msongo wa mawazo baada ya kujifungua," Nadia alisema.

Wanandoa hao walifichua kwamba baada ya takriban wiki mbili, Arrow Bwoy alirudi nyumbani na wakasuluhisha mzozo wao.

"Tulikaa chini tukaongea. Hakuomba msamaha. Alikuja tu akauliza mtoto ako aje," Nadia Mukami alisema.

Arrow Bwoy alisema, "Nilisikia vitu anapitia nikaona sio rahisi. Nikaona nitulie.Sikuwa nampatia wakati wa kuketi chini."

Katika mahojiano hayo, Nadia pia alifichua kuwa alipoteza sauti yake nzuri baada ya kujifungua, jambo lililorudisha nyuma muziki wake.

"Nilipoteza sauti. Mapafu yangu yalisukumwa juu nilipokuwa mjamzito. Sauti yangu haikuwa sawa. Nilikuwa nikijitahidi kurekodi muziki mpya ," alisema.

Alidokeza kuwa mambo mengi ambayo alikumbana nayo baada ya kujifungua yalichangia katika utengano wao wa muda mfupi.