Brian Chira ajibu madai ya kuwa shoga, kuambukizana virusi vya UKIMWI

Mtayarishaji wa maudhui huyo mwenye utata alidai kuwa watu wa jinsia zote wamekuwa wakimmezea mate.

Muhtasari

•Brian Chira alidokeza kuwa hivi majuzi alikuwa kwenye mahusiano na mwanamke ambaye alimtema baada ya kujizolea umaarufu.

•Brian Chira alipuuzilia mbali madai ya kuambukizana virusi hivyo huku akibainisha kuwa anaheshimu hisia za watu.

Mwanatiktok Brian Chira
Image: RADIO JAMBO

Mtumbuizaji maarufu wa tiktok Brian Chira alikuwa mgeni maalum katika kipindi cha Jumanne cha Bustani la Massawe kwenye Radio Jambo ambapo alizungumzia madai ya kuwa shoga.

Brian Chira ambaye ana sifa kadhaa zinazowafanya watu kujiuliza maswali chungu nzima kuhusu jinsia yake halisi aliweka wazi kuwa yeye si shoga na kubainisha kuwa anavutiwa na jinsia tofauti.

Alisema kuwa mara nyingi watu hukisia mambo sana kumhukumu kutokana na sifa zake za kutatanisha.

“Mimi ni straight, niko straight kabisa. Watu wanakisia sana, lakini mimi hupenda sifa tofauti... watu wanakisia juu utaniona na kucha alafu uskie naitwa Chira, mimi ni Brian Chira.. hako kaaccent ni kama msichana,” Chira alimwambia mtangazaji Massawe Japanni.

Mtumbuizaji huyo wa tiktok mwenye utata alidai kuwa watu wa jinsia zote wamekuwa wakimmezea mate.

“Niko na sifa za msichana, hivyo ndo nilizaliwa si ati nikupenda ama nini. Kila mtu ananitaka, nitafanya? Wananitaka wote,” alisema.

Alidokeza kuwa hivi majuzi alikuwa kwenye mahusiano na mwanamke ambaye alimtema baada ya kujizolea umaarufu.

“Niko single saai. Tuliachana juu nilianza kuwa maarufu,” alisema.

Chira ambaye mara nyingi amekiri kwa ujasiri kwamba anaishi na virusi vya ukimwi hata hivyo aliweka wazi kuwa hakuwa akifanya mapenzi bila kinga na mpenzi wake.

Katika mahojiano hayo, mtumbuizaji huyo alisimulia kwamba alipata virusi hivyo baada ya kulawiti alipokuwa akiburudika mjini Mombasa.

"Ni kweli nina ugonjwa wa ukimwi kwa miaka miwili sasa na mimi humeza tembe. Niliambukizwa virusi mjini Mombasa kwa sherehe, nafikiri nililewa sana na nikalaitiwa. Nilipiga ripoti lakini mwenye kunifanyia hivyo alijitoa uhai baada ya wiki mbili," Chira alisema.

Mtayarishaji wa maudhui huyo alipuuzilia mbali madai ya kuambukizana virusi hivyo huku akibainisha kuwa anaheshimu hisia za watu.

"Sio kweli ati nimekuwa nikiambukiza watu kwa kujua. Ninaheshimu watu na hisia za watu," alisema.