Gloria Ntazola ajuta kutumia lugha ya matusi dhidi ya kanjo,anyenyekea na kuomba radhi

Hata hivyo, alisema kwamba angependa baada ya uchunguzi na sakata lote kutulia, angemtafuta ili wapate kufanya mazungumzo ya kusameheana.

Muhtasari

• "Hiyo si tabia yangu kwa kawaida, kutoka nyumbani nilikuwa na hasira zangu kutokana na mwenye nyumba kuongeza kodi ya kila mwezi" alisema.

Ntazola na Kanjo.
Ntazola na Kanjo.
Image: Instagram

Gloria Ntazola, mrembo aliyegonga vichwa vya habari wiki iliyopita baada ya jukwaruzana na askari wa kaunti ya Nairobi maarufu kama Kanjo hatimaye amevunja kimya chake ndani ya kituo cha Radio Jambo.

Ntazola ambaye alikuwa anazungumza kwenye kipindi cha Ilikuwaje na mtangazaji mahiri Massawe Japanni alisema kwa mara ya kwanza kwamba anajutia kwa jinsi alivyoonesha tabia yake ya ukali dhidi ya kanjo huyo aliyekatalia ndani ya gari lake.

Ntazola alisema kwamba hiyo si tabia yake katika maisha ya kawaida na alijuta kutumia lugha ya matusi kwa kanjo, akisema kwamba alikuwa amechochewa na hasira za mwenye nyumba wake ambaye alikuwa awali amewaarifu kupandishwa kwa kodi ya kila mwezi ya nyumba.

“Kusema ukweli ninaomba radhi sana ninajuta kutumia lugha kama ile dhidi yake [kanjo]. Hiyo si tabia yangu kwa kawaida, kutoka nyumbani nilikuwa na hasira zangu kutokana na mwenye nyumba kuongeza kodi ya kila mwezi. Biashara iko chini sana na mtu yeyote anayefanya biashara anaweza kuambia biashara katika siku za hivi karibuni haijakuwa sawa, tunahangaika kupata pesa,” Ntazola alisema.

Mrembo huyo alifichua kuwa ni mjasiriamali anayeendesha maduka mawili ya vipodozi jijini Nairobi lakini pia akafichua kwamba mpaka kuamua kumfanyia kanjo jinsi alivyomfanyia, alikuwa amemtega kwa mara kadhaa.

Ntazola alisema kuwa kanjo huyo aliyemwendesha hadi Kitengela na kumuacha huko si mara ya kwanza alikuwa anamhangaisha kila mara anapoingia jijini na kuanza kutafuta sehemu ya kuegesha gari lake.

Alisema kwamba kwa mara kadhaa walikuwa wamekwaruzana na kanjo yule yule na katika baadhi ya hizo aliwahi kumpa hongo ili kumuachilia, kile alichokitaja kuwa ni kumzoea na akaapa kumpa mzomo wa karne ili kumkoma.

“Niliendesha hadi Kitengela kwa kasi ya 60KPH na nilitumia Expressway kwa sababu sikuwa nataka kusababisha ajali na sikutaka kutumia barabara ya chini ili kukutana na msongamano wa magari. Nilimfikisha hapo karibu na Kitengela nikamwambia sasa shuka utumie nauli yako kurudi,” Ntazola alimwambia Massawe.

Hata hivyo, alisema kwamba angependa baada ya uchunguzi na sakata lote kutulia, angemtafuta ili wapate kufanya mazungumzo ya kusameheana.