Babake Mtumishi avunja kimya baada ya aliyekuwa mkewe kushtumiwa kwa ushirikina na kuvunja familia

Bw. Victor aliweka wazi kwamba hakufurahishwa na maoni ambayo mwanawe alitoa hadharani siku chache zilizopita.

Muhtasari

•Wazazi wote wawili wa Mtumishi walipigiwa simu ili kutoa maoni yao kuhusiana na suala hilo ambalo limekuwa gumzo kubwa nchini Kenya.'

•Bw Victor alifichua kuwa Jumatano walishikiriki kikao cha familia ambapo walikubaliana kuwa mambo ya familia yatasuluhishwa faraghani.

Image: RADIO JAMBO

Siku ya Alhamisi alasiri, mtangazaji Massawe Japanni alimkaribisha mcheshi Gilbert Barasa almaarufu Mtumishi katika kipindi cha Bustani la Massawe kwenye Radio Jambo.

Wakati wa kipindi hicho, wazazi wote wawili wa mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show walipigiwa simu ili kutoa maoni yao kuhusiana na suala hilo ambalo limekuwa gumzo kubwa nchini Kenya katika siku kadhaa zilizopita. Mtumishi amekuwa akivuma sana kwenye mitandao ya kijamii katika kipindi cha siku zilizopita baada ya kusikika akisema mambo ya kushtua kuhusu mamake wakati wa kipindi cha kanisa la Jumapili.

Babake Mtumishi, Bw. Victor alipopigiwa simu, aliweka wazi kwamba hakufurahishwa na maoni ambayo mwanawe alitoa hadharani siku chache zilizopita.

“Alinipigia akaniambia amekwazika moyoni, ikawa kuna mambo fulani alihitaji kutoa moyoni asikie ako huru. Wenzake walipopata hayo maneno, ndio wakaamua kuanika kwenye mtandao,” Bw Victor alisema.

Aliendelea, “Mimi kama mzazi haijanifurahisha kwa sababu huyo ni mkubwa wao. Kuna mambo mengi amewasaidia (ndugu za Mtumishi) nayo kwa hivyo sio vizuri kwa kuwa ni yeye ndiye wanaona mtu mashuhuri kwa vile anafanya mambo moja, mbili alafu aegemee pande moja na aanze kupiga vita upande mwingine. Hilo halikubaliki.”

Bw Victor alifichua kuwa Jumatano walishikiriki kikao cha familia ambapo walikubaliana kuwa mambo ya familia yatasuluhishwa faraghani.

"Kuweka mitandaoni na kujaribu kuharibia mtu jina, hiyo ata mimi sitakubaliana nao," alisema.

Aidha, babake Mtumishi pia aliapa kumtafuta mchekeshaji huyo na ndugu zake ili kujadiliana nao kuhusu tukio la hivi majuzi na pia kuzungumzia jinsi ya kushughulikia masuala ya familia.

Massawe pia alimpigia simu mamake Mtumishi ambaye alisikika kuwa na uchungu sana moyoni huku akilalamika kuhusu hatua ya mwanawe kumsema vibaya hadharani.

“Kwa nini alinipeleka akaniweka kwa ulimwengu mzima? Sitaki kuongea na yeye saa hii! Kama anataka tuongee, akuje nyumbani tuongee mbele ya watu wetu!” Mama Mtumishi alisema kwa sauti yenye ghadhabu sana.

Pia alionekana kutupilia mbali madai ya uchawi ambayo mwanawe aliibua akimtaka aende aonyeshe ushahidi kuthibitisha kuwa ni kweli.

“Kama alisema mimi ni mchawi, basi akuje atoe hayo manyoka. Kama mimi ni mchawi, hata yeye ni mchawi. Wachana na hizo, sitaki kuongea. Kama ni kuzungumza, ni mbele ya wazazi wangu na ndugu zangu, akuje tuongee, sitaki kuongea sasa,” alisema kisha akakata simu mara moja.

Alipopigiwa simu mara ya pili, alizungumza vizuri kuhusu mwanaye na kusisitiza kuwa licha ya yote yaliyotokea, bado mchekeshaji huyo ni mtoto wake.

“Kama uliskia uchungu mbona hukuja? Hata bosi yangu amekuja hapa kuniuliza, unataka kuniharibia kazi nani anilishe,” Mama Mtumishi alimuuliza mwanawe.

Aliongeza, “Tutaongea nyumbani, na sio pekee yangu kabisa, na sio mahali kwingine nyumbani. Wewe ni mtoto wangu. Sina shida na wewe.”

Mtumishi alifurahia kuongea vizuri na mamake baada ya muda mrefu na akasema, “Nimefurahi mama amesema tuende tuongee. Hivyo ndo nilikuwa nataka. Simchukii, nampenda ni mama yangu”