Savara azungumzia kuvunjwa kwa bendi ya Sauti Sol, sababu ya wao kutengana

Hata hivyo, alidokeza kwamba kuna uwezekano wa mashabiki kuwaona tena wakifanya kazi pamoja.

Muhtasari

•Savara ameweka wazi kuwa hawajavunja bendi hiyo ambayo imekuwa mwamba mkubwa katika tasnia ya muziki ya Kenya.

•Alisema mashabiki wao wanapaswa kushukuru kwa muziki na shoo nzuri ambazo wamewapa katika miaka iliyopita .

ndani ya studio za Radio Jambo
Savara ndani ya studio za Radio Jambo

Delvin Savara Mudigi, mmoja wa Sauti Sol ameweka wazi kuwa hawajavunja bendi hiyo ambayo imekuwa mwamba mkubwa katika tasnia ya muziki ya Kenya kwa takriban miongo miwili iliyopita.

Akizungumza siku ya Jumatatu katika mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, msanii huyo mwenye kipaji kikubwa alifichua kuwa bendi maarufu ya Sauti Sol imechukua mapumziko.

Savara alisema yeye na washiriki wenzake wawili wa bendi hiyo waliamua kutengana kwa muda baada ya kuzoeana kiasi kwamba hawakuwa na lingine jipya.

"Nimeishi maisha yangu ya Sauti Sol, mpaka tulikuwa tumefika wakati ambapo tulikuwa tumezoeana sana hadi unapata sileti magic mpya," Savara alisema.

Aliongeza, “Pia kama wanaume waliokomaa, tukaamua bendi huchukua mapumziko. Kwa hiyo, hii si kuvunja bendi. Kuvunja bendi huwa ile ya hata ukitaja Bien hapa ata sitaki kumsikia.”

Msanii huyo ambaye anakusudia kuachia EP yake hivi karibuni alibainisha kuwa mashabiki wao wanapaswa kushukuru kwa muziki na shoo nzuri ambazo bendi hiyo imekuwa ikiwapa katika miaka mingi iliyopita ambayo wamekuwa pamoja.

Hata hivyo, alidokeza kwamba kuna uwezekano wa mashabiki kuwaona tena wakifanya kazi pamoja katika siku za usoni.

"Tunajipanga upya. Ni vizuri kuacha mambo ndio ata mpate uzoefu mpya. Saa hii Sauti Sol vile tutarudi tena tutawapatia vitu tofauti. Ni mapumziko tu kwa sasa,” alisema.

Sauti sol ilitumbuiza kwa mara ya mwisho kabisa kama bendi kwenye matamasha yaliyofanyika tarehe 2 na 4 Novemba mwaka jana.

Huku akizungumza kwenye mahojiano ya pamoja na wanahabari jijini Nairobi kabla ya tamasha hilo, Bien alitajai muda waliokaa pamoja kama ndoa na walihitaji kuwa huru baada ya kuonana kila siku.

“Hii inatokea kwa mara ya 3 ndani ya miaka mitatu imekuwa safari, nilimsikia bibi mmoja akisema ilikuwa ni shoo ya mwisho, sio ya mwisho ni mapumziko tunapumzika, ni mapumziko ya miaka 20 ya kuwa pamoja na kuonana kila asubuhi ni kama ndoa." alisema Bien.