Jay Melody afichua changamoto kubwa katika safari yake ya muziki

Melody aliweka wazi kwamba taaluma yake ya muziki ilingo'a nanga vizuri mwaka wa 2017.

Muhtasari

•Kwenye mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni, Melody aliweka wazi kwamba taaluma yake ya muziki ilingo'a nanga vizuri mwaka wa 2017.

Image: INSTAGRAM// JAY MELODY

Mwimbaji mashuhuri wa Bongo Sharrif Said almaarufu Jay Melody amefunguka kuhusu safari yake ya muziki.

Katika mahojiano na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, Melody aliweka wazi kwamba taaluma yake ya muziki ilingo'a nanga vizuri takriban miaka sita iliyopita baada ya kuwachia kibao 'Goroka'

"2017 nilipata kutoa wimbo 'Goroka' ambao ulinitoa zaidi. Ulitamba sana nchini Tanzania. Mwaka wa 2021 nilitoa 'Huba Hulu' ambao ulipata kuvuma hata hapa Kenya," alisema.

Mwimbaji huyo wa kibao 'Sugar' alikiri kuwa mwanzoni alikabiliwa na changamoto kubwa ya kuwaaminisha watu kuwa anajua kuimba.

"Huwezi kupata favour ya mtu kukupokelea vizuri mwanzoni. Wakati mwingine unaweza kukataliwa kwenye radio," alisema.

Pia alidokeza kuwa alikabiliwa na tatizo la kukataliwa na baadhi ya wasanii wakubwa wakati bado akiwa msanii chipukizi.

"Kuna wasanii wakubwa unajitahidi kufanya kazi nao lakini hawaoni interest. Wakati mwingine unaweza ukaweka vesi yako kwa wimbo kisha ikatolewa kwa sababu bado hujapata kusikika. Lakini sasa siwezi kukataliwa mimi ni msanii mkubwa,"

Katika kipindi hicho, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alifunguka kuhusu upendo wake mkubwa kwa wasanii wa Kenya.

Melody alisema kwamba anawatambua  wasanii wengi wa Kenya na kukiri anapata msukumo mkubwa kutoka kwao.

"Nawapenda watu wengi Kenya. Napata msukumo kwa wasanii wa Kenya. Nawapenda kina Otile Brown, Jovial Mejja, Masauti," alisema.

Alisema kuwa nyimbo za Kenya zinachezwa sana nchini Tanzania hasa jijini Dar es Salaam.

Pia alidokeza kuwa atafanya collabo na msanii wa Kenya hivi karibuni.