Nipo single! Otile Brown aeleza kwa nini hutafuti mchumba baada ya kutengana na Nabbi

Otile alibainisha kuwa hatasita kujitosa kwenye mahusiano mwenzi sahihi akija njia yake.

Muhtasari

•Otile Brown alieleza kuwa mahusiano yake ya awali  yalimfanya kuwa mwangalifu zaidi ifikapo ni suala la mapenzi.

•Brown alishauri kuwa wakati mzuri wa kupata mchumba ni wakati ambapo mtu anajijenga wala sio baada ya kufanikiwa.

katika studio za Radio Jambo baada ya mahojiano mnamo Ijumaa Julai 15, 2022
Otile Brown na Massawe Japanni katika studio za Radio Jambo baada ya mahojiano mnamo Ijumaa Julai 15, 2022
Image: RADIO JAMBO

Staa wa Swahili RnB Jacob Obunga almaarufu Otile Brown amekiri kwamba hachumbiani na mtu yeyote kwa sasa. 

Akihojiwa kwenye shoo ya Bustani la Massawe siku ya Ijumaa, msanii huyo aliyebarikiwa na kipaji kikubwa pia aliweka wazi kuwa hayupo kwenye harakati za kutafuta mchumba.

Alidai kuwa si rahisi kwake kupata mpenzi sahihi katika nafasi aliyopo kwa sasa na hivyo anachukua muda wake.

"Nipo single saa hii. Nachukua muda wangu. Ni ngumu kwangu. Mimi kuwa katika nafasi hii kwa sasa siwezi kujua ambaye ninakutana naye kama ni mkweli au la," Alisema Otile

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alieleza kuwa mahusiano yake ya awali  yalimfanya kuwa mwangalifu zaidi ifikapo ni suala la mapenzi.

"Kila mtu ambaye anakuja inakuwa lazima namhakiki. Ni kama unawaangalia kweli anaweza ama hawezi. Labda utakuta kuna vitu amefanya unaona huyo sio yeye. Ni mtihani mkubwa," Alisema.

Licha ya kuwa kwa sasa hatafuti mchumba, Otile alibainisha kuwa hatasita kujitosa kwenye mahusiano ikitokea mwenzi sahihi akija njia yake.

"Sitafuti kabisa. Nachukua muda wangu. Nataka awe ametumwa kwenye njia yangu. Huwezi kutafuta mwenzi wako. Ni ngumu sana,"

Aidha alishauri kuwa wakati mzuri wa kupata mchumba ni wakati ambapo mtu anajijenga wala sio baada ya kufanikiwa.

Haya yanajiri siku chache tu baada yake kuwa anammezea mate sana mwimbaji wa R&B Toni Braxton.

Brown alieleza hisia zake kwa Braxton kwenye Instagram na  kumtambua mama huyo wa watoto wawili kama kiumbe maalum cha Mungu.

"Bado namcrushia.. Mmoja wa wanawake wazuri zaidi ambao Mungu aliwahi kuumba," Brown aliandika.

Mwezi Januari Otile alitangaza kuvunjika kwa mahusiano yake ya miaka mitatu na kipusa Nabayet kutoka Ethiopia.

"Mimi na Nabbi hatuko pamoja tena. Mara ya mwisho tulikuwa pamoja ilikuwa kujaribu kutafuta njia ya mbele lakini tuliamua kwenda tofauti kwa bahati mbaya," Brown alitangaza kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Licha ya kutengana kwao, Brown alieleza kwamba yeye na malkia huyo kutoka Ethiopia wangeendeleza uhusiano mzuri.