"Sikuzaliwa hivi!" Seneta Crystal Asige afunguka alivyogeuka kuwa kipofu akiwa kijana

Seneta Crystal Asige amefichua kwamba alizaliwa akiwa na uwezo kamili wa kuona.

Muhtasari

•Crystal aligundua shida yake ya macho alipoanza kuwa na matatizo ya kuona ubao, kusoma na kufanya mambo mengine ambayo yalihitaji kuangalia kwa makini.

•Crystal alifichua alikuwa na wakati mgumu kukubali hali yake mpya na kukubali maisha yake mapya baada ya kutoweza kuona tena.

Image: INSTAGRAM// CRYSTAL ASIGE

Seneta maalum wa Kenya, na ambaye alikuwa msanii wa Sol Generation, Crystal Asige amefichua kwamba alizaliwa akiwa na uwezo kamili wa kuona.

Katika mahojiano ya kipekee na mtangazaji Massawe Japanni kwenye Radio Jambo, Crystal ambaye aliteuliwa katika seneti mwaka jana kuwakilisha watu wanaoishi na ulemavu alifichua kwamba alitambua hali yake ya macho alipokuwa na umri wa karibu miaka kumi na minne.

“Sikuzaliwa hivi, nilikuwa na macho kamili nilipozaliwa. Lakini nilifika mahali katika shule ya upili nikiwa na umri wa karibu miaka 14-15 ndio nilianza kuona kuna shida na macho zangu, nikawasioni vizuri,” Crystal Asige alisema.

Mwimbaji huyo mwenye sauti nyororo alisema aligundua shida yake ya macho alipoanza kuwa na matatizo ya kuona ubao, kusoma na kufanya mambo mengine ambayo yalihitaji kuangalia kwa makini.

"Niliona gizagiza wakati huo. Nikasema, “Okay, mama anavaa miwani, mzee anavaa miwani, labda ni miwani tu nahitaji.” Kwa hiyo nikaenda kwa daktari wa macho akaniambia sihitaji miwani pekee, kuna shida na macho zangu huko nyuma,” alisimulia.

Crystal alisema kwamba baada ya kufanyiwa vipimo vingi vya macho kwa miaka mingi, madaktari wa macho hatimaye walibaini kuwa alikuwa na ugonjwa unaoitwa ‘Glaucoma.

“Glaucoma ni shida ya macho ambayo inahusisha shinikizo kwenye macho. Sio shinikizo la damu ambalo tumezoea kuskia, ni shinikizo kwenye jicho ambayo ikiwa juu sana, inakula jicho hivyo kukosa uwezo wa kuona. Inaenda polepole tu, sio ati ni kitu ambacho kinatokea leo alafu kesho unaona tofauti. Ni polepole sana, inachukua miaka mingi," alielezea.

Mwimbaji huyo alieleza kuwa hali yake iliendelea kukithiri alipokuwa kati ya miaka 15-21 na hatimaye akageuka kuwa kipofu kabisa.

Crystal alifichua kwamba alikuwa na wakati mgumu kukubali hali yake mpya na kukubali maisha yake mapya baada ya kutoweza kuona tena.

“Ilikuwa ngumu. Usiku mwingi nililia, nilikuwa naomba. Namuuliza Mungu mbona mimi? Hasa kwa sababu alinipa uwezo wa kufanya muziki, jukwaani, kuwa muigizaji. Nilipenda vitu hivyo. Siku zote nilikuwa nikipigana na Mungu lakini ilifika wakati Mungu akaniambia nitulie. Tangu siku hiyo nimehakikishiwa kuwa Mungu ananilinda,” alisema.

Crystal hata hivyo alisema kuwa kwa sasa tayari amekubali hali yake na amejifunza kukimbiza ndoto zake licha ya kutokuwa na uwezo wa kuona.