Yesu wa Tongaren aeleza kwa nini anakwepa kusulubiwa wakati wa Pasaka

Bw Simiyu amekanusha madai kuwa kwa sasa anajificha ili kuepuka kusulubiwa.

Muhtasari

•Yesu wa Tongaren alibainisha kuwa kusulubiwa kulitokea tu kwa Yesu Kristo wa asili, karne 20 zilizopita wakati wa ujio wake wa kwanza duniani.

•"Kusulubiwa sasa naona haikubaliki kwa sheria ya Mungu. Hiyo iliisha," alisema.

Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Yesu wa Bungoma azungumzia kusulubishwa pasaka
Image: Maktaba

Mchungaji mwenye utata kutoka kaunti ya Bungoma, Eliud Simiyu almaarufu Yesu wa Tongaren amekanusha madai kwamba kwa sasa anajificha ili kuepuka kusulubiwa wakati wa msimu ujao wa Pasaka.

Akizungumza wakati wa mahojiano ya simu na mtangazaji Massawe Japanni, Yesu wa Tongaren alibainisha kuwa kusulubiwa kulitokea tu kwa Yesu Kristo wa asili, karne 20 zilizopita wakati wa ujio wake wa kwanza duniani.

Alisema kwamba kwa sasa mambo yamebadilika sana na kusulubiwa ni kinyume na sheria ya ulimwengu wa sasa.

"Hiyo ilikuwa miaka 2000 iliyopita. Katika kizazi hiki cha sasa, hilo jambo limepitwa na wakati. Kila kitu kinachotendeka ni lazima kiwe chini ya sheria. Iwapo hakipo, itakuwa ni kuvunja sheria," alisema.

Baba huyo wa watoto wanane alitumia mstari wa Biblia katika kitabu cha Waebrania 9:27-28 kueleza kwamba ujio wa pili wa Yesu Kristo ulisemekana kuwa kwa minajili ya kuwachukua wale wanaomngoja wala sio kuwaokoa wale wenye dhambi kama ilivyokuwa katika kuja kwake mara ya kwanza.

"Kusulubiwa sasa naona haikubaliki kwa sheria ya Mungu. Hiyo iliisha," alisema.

Wakati wa Mahojiano, Massawe Japanni alikataa kabisa kumwita Bw Simiyu 'Yesu.'  Huku akimjibu, mchungaji huyo anayeishi Tongaren alimtishia kuwa pia yeye atamkana mbele ya babake watakapofika mbinguni.

"Imeandikwa, walionikana mbele ya watu wengi, pia mimi nitawakana mbele ya Baba yangu na malaika," alisema.

Bw alifichua kuwa alizindua kanisa lake 'Kanisa la Yesu' mwaka wa 2009 na ameendeleza  injili kwa zaidi ya mwongo mmoja uliopita. Alisema kuwa kanisa lake lina manabii kumi na wawili pamoja na washirika wengine.

Pia aliweka wazi kuwa ameweza kutembela katika mataifa yote duniani kiroho katika harakati za kuendeleza neno la Mungu.

"Saa hii nimezunguka mataifa yote ya dunia kiroho na hata walimwengu wananitazama sasa kwenye runinga," alisema.

Kabla ya kutoka hewani, Yesu wa Tongaren alitabiri kuwa jambo kubwa linaenda kutokea nchini Kenya ambapo mataifa mengi yatakusanyika kushuhudia.