Nyakati nzuri huku Gidi akishangaza bintiye kwa maendeleo makubwa katika kujifunza Kifaransa (+video)

Mtangazaji huyo alianza kujifunza Kifaransa baada ya kuchekwa na bintiye.

Muhtasari

•Gidi alimfahamisha Marie-Rose kuhusu maendeleo yake kwa kutamka baadhi ya maneno ya ambayo amefanikiwa kujifunza.

•Mtangazaji huyo alijitambulisha kwa bintiye kwa Kifaransa ili kumthibitishia kuwa anajua kuzungumza lugha hiyo.

Image: INSTAGRAM// GIDI OGIDI

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi kwenye Radio Jambo, Gidi Ogidi amefurahishwa na maendeleo yake katika kujifunza Kifaransa.

Siku ya Jumatano, mwanamuziki huyo wa zamani alimfahamisha binti yake Marie-Rose kuhusu maendeleo yake katika kujifunza lugha hiyo ya kigeni kwa kutamka baadhi ya maneno ya ambayo amefanikiwa kujifunza.

"Alishtuka sana kwamba hatimaye baba yake anaweza kuzungumza Kifaransa," Gidi alisema chini ya video ya mazungumzo ya mtandaoni na bintiye ambayo alichapisha  kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Katika mazungumzo yao, mtangazaji huyo alijitambulisha kwa bintiye kwa Kifaransa ili kumthibitishia kuwa anajua kuzungumza lugha hiyo.

Marie-Rose ambaye kwa sasa anaishi na mama yake nchini Ufaransa na alionyesha mshangao mkubwa baada ya kumskia babake akiongea Kifaransa. Pia alichukua jukumu la kumrekebisha alipotamka maneno fulani kimakosa.

"Hujachelewa kuanza changamoto maishani, @afnairobi imerahisisha kujifunza Kifaransa kwa madarasa yao ya mtandaoni ya kila siku," alisema.

Mapema mwezi huu,  Gidi alianza jaribio lake la nne la kujifunza lugha ya Kifaransa baada ya kushindwa katika majaribio yake matatu ya awali.

Katika tangazo lake, mtangazaji huyo mahiri alieleza matumaini yake kuwa mara hii hatimaye atafanikiwa kusoma lugha hiyo ya kigeni.

"Hili litakuwa jaribio langu la 4 lakini safari hii nina matumaini kuwa nitafanikiwa," alisema kwenye mtandao wa Instagram.

Mtangazaji huyo alifichua kuwa safari yake ya nne ya kujifunza Kifaransa ilianza baada ya kuchapisha video ya binti yake, Marie-Rose, akijaribu kumfundisha lugha hiyo takriban  miezi miwili iliyopita.

"Watu wengi walionitakia heri nchini Ufaransa na Kenya walijitolea kunisaidia kujifunza Kifaransa. Hatimaye nilifuatiliwa kupitia Ubalozi wa Ufaransa na Alliance Francaise ambao wametoa mpango wa ushirikiano kujifunza Kifaransa," alisema.

Katika video iliyochapishwa mwezi Januari, Marie-Rose alionekana akimfundisha baba yake maneno ya Kifaransa. Rose alicheka sana lafudhi ya baba yake alipokuwa akijaribu kurudia maneno ya Kifaransa baada yake.

Gidi alifichua kuwa anakusudia kumshangaza binti huyo wake mdogo kwa ubabe wake wa Kifaransa katika muda wa miezi michache ijayo baada ya kuanza masomo katika Alliance Francaise siku ya Jumatatu.

"Nimekuwa nikijaribu kuja hapa kuanza masomo yangu kisha ninaacha. Nina matumaini kwamba wakati huu nitafanya vyema," alisema.