Patanisho: 'Bwanangu alisema angeniua nirudi kwetu nikiwa kwa sanduku' Mwanadada asimulia alivyogura kwa ndoa miaka 8 iliyopita

Muhtasari

•Kamau, ambaye ilikuja kufahamika baadae kuwa jina lake rasmi ni Ngatia alieleza kwamba mkewe alitoroka nyumbani baada ya kuzozana na mama mkwe kuhusiana na suala la shamba

•Bi Njeri alipopigiwa simu alieleza kuwa alisikitika baada ya mumewe kukosa kuchukua hatua wakati mama mkwe alikuwa anamtupia maneno makali.

•Njeri alifichua kwamba mumewe aliwahi kutishia kumuua baada yake kulalamika kuhusu mama mkwe na hapo ndipo aliamua kutoroka.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Peter Kamau (40) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa  na mke wake Damaris Njeri (27) ambaye walitengana miaka nane iliyopita.

Kamau, ambaye ilikuja kufahamika baadae kuwa jina lake rasmi ni Ngatia alieleza kwamba mkewe alitoroka nyumbani baada ya kuzozana na mama mkwe kuhusiana na suala la shamba.

Kabla ya kutengana, wawili hao walikuwa wamekaa kwa ndoa kwa kipindi cha miaka mitatu na kubarikiwa na watoto wawili.

"Tulikuwa tunakaa kwa shamba ya 50*100. Mama amejenga kwa kona moja nami nimejenga kwa kona nyingine. Mama na mke wangu walikosana kwa sababu ya bustani ya jikoni ambapo mke wangu alikuwa amepanda mboga na vitunguu.

Kwa vile mama yangu hakuwa na kitunguu alienda akachuna matawi kadhaa na akapika. Mke wangu aliporudi nyumbani na kuona kuwa vitunguu vyake vilikuwa vimechunwa alikasirika na kumgombeza mama. Alimuuliza nani alikuwa amempa ruhusa ya kuchuna kitunguu. Mama alikasirika kidogo akamwambia kuwa shamba ile ni yake eti hafai kuulizwa swali na yeyote. Ploti ni ya mama, mimi nimejenga kwa mama" Kamau alisimulia.

Kamau alisema kwamba baada ya tukio hilo mvuragano kati ya mkewe na mama yake uliendelea kuwa mkubwa zaidi kila siku hadi siku moja akaamua kurudi kwao.

"Mimi sikuwa akienda. Nilipomuuliza aliniambia kuwa walikosana na mama. Nilipendekeza tuhame ila akakataa. Watoto wako kwa mama yake ila yeye alienda kutafuta kibarua kwingine. Hapo awali nilijaribu kumshawishi ila nikashindwa" Kamau alisema.

Alisema kuwa alikuwa ameficha jina lake la ukweli kwa kuwa alihofia maswali mengi kutoka kwa familia na majirani kufuata baadae kwa kuwa wengi wao ni mashabiki wakubwa wa Radio Jambo. Hata hivyo ilibidi afichue jina lake mkewe alipopigiwa simu.

Bi Njeri alipopigiwa simu alieleza kuwa alisikitika baada ya mumewe kukosa kuchukua hatua wakati mama mkwe alikuwa anamtupia maneno makali.

Alifichua kwamba mumewe aliwahi kutishia kumuua baada yake kulalamika kuhusu mama mkwe na hapo ndipo aliamua kutoroka.

"Mara ya kwanza alinikujia na nikarudi. Mamake hakufurahia akaniuliza mbona nikarudi ilhali tulikuwa tumekosana. Mama yake alinitukana yeye akiwa ameketi hapo chini. Alisikia kila kitu ila hakuchukua hatua. 

"Tulikosana na yeye kwa kuwa niliambia mama yangu kuwa mama mkwe aliniambia kila anaponiona kwa boma yake huwa anaona nikiwa maiti. Aliniambia ataniweka kwa sanduku niende kwetu nikiwa kwa sanduku. Mungu alinisaidia, akienda kuchukua panga nikatumia nguvu zangu nikamuweka kwa kiti nikatoroka.

Nilivumilia mwezi mzima. Siku tuliyokosana  nilikuwa nimemuitisha pesa za kununua makaa nipikie watoto. Alianza kunigombanisha na kunichapa kisha akaniambia ni kwa sababu niliambia mama yangu yale ambayo mama mkwe aliniambia.  Aliniambia ningeenda kwetu nikiwa maiti. Nilipigia ndugu yangu simu anichukue mjini" Njeri alisimulia.

Njeri alidai kuwa hakuna uwezekano wake kurudi kwa Kamau huku akimshtumu kwa kutelekeza watoto wao.

Alifichua kuwa Kamau alikuwa ameoa wake watatu tangu alipoondoka pale mwaka wa 2013.

Kamau alikubali kusaidia watoto wake kusoma