Patanisho: "Huwezi kula chakula moja tu!" Jamaa ajitetea baada ya mkewe kumfumania na mpango wa kando kitandani

Muhtasari

•Moraa alisema kuwa alikuwa ametoka sokoni wakati alipofumania mumewe na mwanamke mwingine wakiwa uchi wa mnyama katika kitanda chao cha ndoa. 

•Makori alipopigiwa simu alidai kuwa aliamua kutafuta mpango wa kando ili kulipiza kisasi kwani aliwahi fumania mkewe na jamaa mwingine.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi, mwanadada aliyejitambulisha kama Mary Moraa 23, kutoka Kisii alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake  Sam Makori 26, ambaye walikosana mwaka wa 2018.

Moraa alieleza kwamba ndoa yao ya miaka miwili ilifika kikomo alipomfumania mumewe na mpango wa  kando ndani ya nyumba yao.

Moraa alisema kuwa alikuwa ametoka sokoni wakati alipofumania mumewe na mwanamke mwingine wakiwa uchi wa mnyama katika kitanda chao cha ndoa. 

"Ilikuwa mwendo wa saa nne asubuhi nikatoka nikaenda sokoni. Kurudi nikapata mume wangu na mwanamke kwa nyumba kama wamelala. Nilikuwa nimeenda kuchukua vitu vya kuuza, alifikiri ningerudi tu masaa ya kawaida ila hiyo siku nilirudi mapema. Nilipofika kwa nyumba nilipata kama mlango imefungwa nikagonga mlango, kuingia nikapata watu wako uchi kitandani. Mimi nilitoka nikamwambia aendelee kukaa na huyo mwanamke nikaenda kwetu. Sikubeba manguo, nilibeba watoto. Ile mboga na nyanya nilikuwa nimebeba nikamwachia nikamwambia aendelee maisha nayo. Nilichukua watoto tu nikatoka hapo nikaenda kwetu kisha nikaenda kufanya kazi Eldoret" Moraa alisimulia.

Alisema kuwa tangu kutengana kwao miaka mitatu iliyopita hawajawasiliana na mumewe ila wiki moja iliyopita alimpigia simu akidai mtoto mmoja ambaye walipata pamoja naye. Alidai kwamba angependelea mahusiano yao yarejee ili waweze kulea watoto wao pamoja.

Makori alipopigiwa simu alidai kuwa aliamua kutafuta mpango wa kando ili kulipiza kisasi kwani aliwahi fumania mkewe na jamaa mwingine.

Hali kadhalika Makori alidai kwamba  mwanaume hawezi kutoshelezwa na mwanamke mmoja na ndiposa akaamua kutafuta mwanamke mwingine.

"Wewe ndio ulitangulia kutengana. Kunipata na mwanamke mwingine kuna shida gani? Huwezi kula chakula moja" Makori aliambia mkewe.

"Niliamua kulipiza kisasi. Mbona yeye akafanya hivo? Pia mimi nilikuwa nimetoka kuenda kazi kurudi nikasikia fununu eti mke wangu anarandaranda na mabwana za watu. Niliposikia hivo, siku moja nikaamua kutoka kuenda kazini. Kurudi masaa ya jioni nilimpata na mwanaume" Makori alisema.

Hata hivyo Moraa alipuuzilia mbali madai ya mumewe huku akisema kuwa zilikuwa fununu tu bila msingi wowote.

Habari njema ni kuwa wawili hao walikubali kusameheana na kurudiana huku Makori akikubali kumtumia Moraa nauli ili aweze kurejea nyumbani.

Ghost aliwahimiza wanandoa hao washiriki mazungumzo baada ya kurudiana ili kujua namna watakavyoendeleza uhusiano wao huku akiwashauri wavumiliane kuona kwamba wangali na umri mdogo.