Patanisho: 'Bwanangu aliniambia ataoa mke mweupe ili asisumbuke kutafuta mwangaza kwa nyumba' Mwanadada asimulia masaibu aliyopitia kwa ndoa

Muhtasari

•Wafula alieleza kuwa mkewe alikosana na mama yake akaondoka nyumbani kwao mwezi Agosti baada yao kuwa kwa ndoa kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.

•Esther alifichua kwamba hakuwa amekosana tu na mama mkwe bali pia na mumewe kwa kuwa alikuwa na mipango wa kando.

•Esther alisema kwamba mumewe alikuwa ameingiza madharau mengi kiasi cha kwamba alianza kumuonyesha picha za wanawake wengine akidai kuwa hao ndio angeoa.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwendesha boda boda  aliyejitambulisha kama Brian Wafula  (24)  kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Esther Abongo (23) ambaye walikosana takriban miezi miwili iliyopita.

Wafula alieleza kuwa mkewe alikosana na mama yake akaondoka nyumbani kwao mwezi Agosti baada yao kuwa kwa ndoa kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.

Jamaa huyo alisema kwamba baada ya mkewe kuondoka nyumbani mama yake alikataa kumweleza yaliyokuwa yametukia kati yake na mkaza mwana wake.

"Walikosana na mama yangu. Walikuwa wanagombana tu sikujua kilichokuwa kinaendelea. Nilipotoka kazi nilipata kama amebeba kila kitu ameenda. Alibeba manguo yake akaenda. Tulikuwa tunazungumza hapo awali lakini sasa ameniblock kwa wiki moja hivi. Naumia sana ndani ya moyo wangu. Mama yangu ni mkali sana na huwa anakunywa,sijui waliongea nini. Nikimuuliza anakuwa mkali" Wafula alisema.

Esther alifichua kwamba hakuwa amekosana tu na mama mkwe bali pia na mumewe kwa kuwa alikuwa na mipango wa kando.

Alisema kwamba familia ya mumewe haikuridhishwa na hatua ya mumewe ya kuoa mke ambaye alikuwa na mtoto mmoja tayari. Jambo hilo lilisababisha malumbano makubwa katika ndoa yao.

"Brayo vile alinioa tulikuwa tunakula kwao. Mama yake na dadake walianza kuleta shida wakiuliza kwa nini Brayo aliamua kuoa mwanamke akiwa na mtoto ambaye si wa damu. Ilileta shida hadi mama yangu akakujia mtoto ili tukae kwa amani" Esther alieleza.

Esther alidai kuwa mama ya mumewe alikuwa na kumtupia matusi makali baada ya kunywa mvinyo hadi akashindwa kuvumilia tena pale nyumbani kwao.

Baada ya tukio hilo wapenzi hao wawili waliondoka nyumbani kwa wazazi wa Wabwire na wakatafuta nyumba ya kukodisha. 

Masaibu zaidi yalikumba ndoa yao baada ya Wafula kuanza kufanya kazi ya bodaboda kwani alianza kujihusisha na mambo ya mipango ya kando.

"Mama yake akilewa alikuwa anakuja ananitusi hadi hamu ya kula chakula inapotea. Nilitoka nikaenda kwetu. Brayo tena akanifuata. Mamangu alipoona hivo alitupea kila kitu tuende tuanze kupika, tukapewa tukaenda. 

Tulipoenda Brayo alipata pikipiki akaanza kufanya kazi ya boda. Aliandika namba yake kwa reflector alafu wateja wake wote walikuwa wasichana. Walikuwa wanatumiana jumbe za simu hadi usiku. Nilipomuuliza alianza kuwa mkali. Hiyo ndio ilifanya nikashindwa kuvumilia nikatoka nikaenda" Esther alisimulia.

Alisema kwamba mumewe alikuwa ameingiza madharau mengi kiasi cha kwamba alianza kumuonyesha picha za wanawake wengine akidai kuwa hao ndio angeoa.

"Alisema kwa sababu huyo mwanamke ni mweupe akiwa kwa nyumba hatashughulika na mambo ya mwangaza. Alafu ameficha jina, anaitwa Wafula" Esther alisema.

Hata hivyo mwanadada huyo alisema kwamba tayari alikuwa amemsamehe Wafula ila alihitaji muda wa takriban mwaka mmoja ili ajipange kwanza.

Baada ya Ghost kujaribu kushawishi Esther ampunguzie Wafula muda, alikubali kupunguza ila akaonye Wafula asimpeleke haraka.