"Watu walisema bwanangu ni mzee sana, sikuweza kutembea naye juu walinicheka" Mwanadada akiri sababu za kugura ndoa

Muhtasari

•Nafula alieleza kwamba aliikimbia ndoa yake kufuatia kejeli nyingi za majirani kuwa alikuwa ameolewa na mzee.

•Mwanadada huyo alikiri kuwa baada ya kumtema mumewe alienda akaolewa na barobaro mwenye umri wa miaka 34 ila baada ya mwezi mmoja tu akagundua kuwa alikuwa anatumiwa tu kama mpango wa kando kwani jamaa yule tayari alikuwa na mke mwingine.

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Irene Nafula (30) alituma ombi akiomba kupatanishwa na mume wake Andrew Munaya (42) ambaye walikosana mwaka wa 2019.

Nafula alieleza kwamba aliikimbia ndoa yake kufuatia kejeli nyingi za majirani kuwa alikuwa ameolewa na mzee.

"Nilioleka na tukaishi tu vizuri lakini watu walikuwa wananicheka eti bwanangu ni mzee sana kunishinda. Mimi mwenyewe nikaamua kutoka, hakuwahi nikosea. Niliona tu ata huwezi tembea na yeye watu wanakucheka" Nafula alisema.

Mwanadada huyo alikiri kuwa baada ya kumtema mumewe alienda akaolewa na barobaro mwenye umri wa miaka 34 ila baada ya mwezi mmoja tu akagundua kuwa alikuwa anatumiwa tu kama mpango wa kando kwani jamaa yule tayari alikuwa na mke mwingine.

Nafula alidai kwamba alimpenda Andrew sana ila akashindwa kustahimili vicheko na kejeli za wamama waliosema mumewe ni mzee sana.

"Alikuta kama nimeenda. Nataka kumuomba msamaha turudiane vile tulikuwa tunaishi. Huwa ananiambia eti ataniambia. Hajapata mke mwingine bado juu ata nikimflash saa sita usiku bado atanipigia. Kama alipata mke ni sawa tu, kama hajapata anisamehe turudiane. Nilimpenda sana, sikujua ana miaka 42, alikaa kijana kijana tu. Nimeona sitakuwa naskiza maneno ya watu" Nafula alisema.

Andrew alipopigiwa simu alithibitisha kuwa mkewe aliondoka nyumbani bila kukosana naye baada ya kusikiza maneno ya watu. 

Ingawa alikiri kuwa bado hajapata mke mwingine, alisisitiza kwamba anahitaji muda zaidi wa kufikiria iwapo atakubali kurudiana na Nafula.

"Alinikosea sana ndio maana nasema nitafikiria" Andrew alisema.

Baada ya juhudi kubwa za Ghost kumshawishi Andrew afanye uamuzi, hatimaye alikubali Nafula aende wapatane siku ya Jumatatu ili wazungumze zaidi.