Patanisho:Jamaa atemwa na mkewe kwa kukosa kumpikia chajio

Muhtasari

•Muyale alisema malumbano makubwa yalianza jioni moja baada ya mke wake kurejea nyumbani na kupata kuwa hakuwa amepika chochote.

•Alifichua kwamba alipandwa na mori na akamgonga mkewe na kumtupa chini, jambo ambalo lilimsukuma afunge virago vyake na akarudi kwao Kakamega.

•Muyale alisema wakati walikuwa katika ndoa alikuwa anafanya majukumu yote ya nyumbani ikiwemo kupika kwa kuwa mke wake alikuwa anatoka kazini akiwa amechelewa.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Aggrey Muyale (24) kutoka Siaya alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mildred (20) ambaye alidai alimuacha mwezi uliopita.

Muyale alisema mzozo uliosababisha kusambaratika kwa ndoa yao ya miaka mitatu ulianza wakati Midred alimuacha kwa nyumba akiwa mgonjwa sana.

Alisema malumbano makubwa yalianza jioni moja baada ya mke wake kurejea nyumbani na kupata kuwa hakuwa amepika chochote.

"Vile nilikuwa mgonjwa nikamwambia sijihisi vizuri. Akatoka kwa nyumba akijua vizuri sihisi vizuri. Sikupika, aliporudi kwa nyumba akaanza makelele mingi akiuliza nilichokuwa nimepika ili akule. Nilikuwa  tu nimelala kwa kitanda nikitetemeka juu nilikuwa nahisi baridi nikamwambia nilikuwa nimemeza dawa tu na strungi sikuwa nimepika chochote" Muyale alisimulia.

Muyale alisema vita ilianza wakati mabishano yao yalikithiri na wakaanza kutupiana maneno makali.

Alifichua kwamba alipandwa na mori na akamgonga mkewe na kumtupa chini, jambo ambalo lilimsukuma afunge virago vyake na akarudi kwao Kakamega.

"Aliniomba simu akaniambia eti anataka kumulika aendee maziwa. Tukaanza kujibizana nikaamka nikamrusha vibaya akaanguka chini karibu na kabati. Alikuwa ananiongelesha kwa madharau. Akatoka akaenda kwao" Alisema Muyale.

Muyale alisema wakati walikuwa katika ndoa alikuwa anafanya majukumu yote ya nyumbani ikiwemo kupika kwa kuwa mke wake alikuwa anatoka kazini akiwa amechelewa.

"Nilikuwa nafanya kila kitu mpaka kupika. Alikuwa anakaa na simu yangu. Nilikuwa napika mpaka nakata mboga, kila kitu nilikuwa namfanyia. Hayakuwa makubaliano, alikuwa anatoka kazini akiwa amechelewa. Singeweza kumngoja eti afike nyumbani aanze kutafuta mboga  na apike. Nilikuwa najua akitoka kazini atakuwa amechoka" Muyale alieleza.

Alisema aliamua kumsaidia mkewe na kazi za nyumbani kwa sababu alimpenda na kumjali sana haswa kwa kuwa alikuwa anarudi kwa nyumba akiwa amechelewa.

Juhudi za Gidi kumfikia Mildred ziliangulia patupu kwani simu yake ilikuwa mteja.

Hata hivyo Muyale alimuomba mkewe msamaha hewani huku akimwomba arudishe roho yake chini ili waweze kurudiana na kusihi pamoja.