Goal! Goal! Mwanadada acheza jamaa baada ya kumpata na mpango wa kando

Muhtasari

•  Kipngetich alisema wamekosana na mke wake mara kadhaa  baada ya wote wawili kukanyanga nje ya ndoa.

•Kipng'etich alisema alijaribu kumsihi mke wake akome kulipiza kisasi ila jitihada zake zote ziliangulia patupu kwani Mama Bravin alikataa kuzungumza naye na hatimaye akaondoka.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama William Kipng'etich (32) kutoka Eldoret alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake  Mama Bravin (25) ambaye walitengana kufuatia mzozo kuhusu udanganyifu kwa ndoa.

 Kipngetich alisema wamekosana na mke wake mara kadhaa  baada ya wote wawili kukanyanga nje ya ndoa.

Alieleza kuwa mke wake ndiye alikuwa wa kwanza kumnasa na mpango wa kando na kufuatia hayo  akaamua kulipiza kisasi kwa kukanyanga nje ya ndoa pia.

"Tulipokuwa kwenye mahusiano tulitengana mara ya kwanza aliponipata na mpango wa kando. Nilipatikana mara ya kwanza alafu ikafika mahali nikawacha naye akaanza. Ilifika mahali akaenda kwao nami nikabaki. Tulirudiana kwa sababu ya watoto. Nilimwambia arudi tuishi na watoto. Alikuja tukakaa na yeye kidogo. Niligundua kuwa bado kuna watu alikuwa anaongea nao kwa simu" Kipngetich alisimulia.

Kipng'etich alisema alijaribu kumsihi mke wake akome kulipiza kisasi ila jitihada zake zote ziliangulia patupu kwani Mama Bravin alikataa kuzungumza naye na hatimaye akaondoka.

Alisema mkewe alipoondoka alitafuta nyumba kwingine na akasita kurudi licha ya majaribio mengi ya kumshawishi arudi.

"Nilimwambia kwa kuwa alikuwa ashalipiza kisasi sasa tutulie tuishi kama familia. Hakusema lolote. Ilifika mahali hakutaka kuzungumza na mimi. Alienda kazini akakosa kurudi. Nikamuuliza kwani alienda kulala wapi alafu tukajibizana kwa jumbe nikamtumia manguo. Alienda akachukua manguo. Ijumaa wiki iliyopita tulizungmza kupitia mzazi wake akasema atarudi. Bado moods zake hazijarudi sawa" Kipngetich alisema.

Kipngetich alikiri kwamba ana mapenzi makubwa sana kwa Mama Bravin huku akiahidi kuendea watoto wao wawili iwapo angekubali kurudi.

Mama Bravin alipopigiwa simu alikataa kabisa kurejea kwa ndoa huku akifichua kwamba Kipngetich aliwahi omba kupatanishwa tena katika Patanisho mwaka uliopita.

Alimwabia Kipngetich asonge mbele na maisha yake kwani hakuna uwezekano wa ndoa yao kufufuka.