Patanisho: Mwanadada agura ndoa ya miaka nne baada ya kupata kazi katika duka kubwa

Muhtasari

•Kirwa alisema anahofia huenda mkewe alinyakuliwa na jamaa mwingine mjini Eldoret ambako alienda kufanya kazi.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho jamaa aliyejitambulisha kama Philip Kirwa (27) kutoka Nandi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Jackline Kiptanui (24) ambaye walikosana mwaka mmoja uliopita.

Kirwa alisema ndoa yake ya miaka minne ilianza kuyumba baada ya mkewe kupata kazi katika duka moja kubwa mjini Eldoret kwani na mawasiliano katika mahusiano yao yakaanza kubadilika.

Alisema Jackline aliondoka nyumbani mnamo mwezi Machi mwakani na hajawahi kurejea tena tangu wakati huo.

Kirwa alisema amekuwa akimpigia mkewe simu katika jaribio la kumshawishi arudi ila kila mara amekuwa akimpatia ahadi za uongo.

Kirwa alikiri kuwa bado hajafunga ndoa rasmi na Bi Jackline ila akasema tayari alikuwa akipanga kuenda kuona wazazi wao hivi karibuni.

"Bado hatujaoana rasmi. Nilikuwa napanga labda  hii Desemba kama angekuwa tuongee vizuri ningekuwa naenda kwao. Ata nilikuwa nimependekeza tutaenda kwao mwezi huu akaniambia aende nyumbani kwanza ndivyo awaambie tupange. Sasa hajawahi kurudi siwezi  jua"  Alisema Kirwa

Kirwa alisema anahofia huenda mkewe alinyakuliwa na jamaa mwingine mjini Eldoret ambako alienda kufanya kazi.

Alisema hajaona mkewe kwa kipindi kirefu kwani amekuwa akiishi kwao tangu mwezi Machi alipogura ndoa yao.

"Amekuwa akiishi kwao. Kwangu ni kama no go zone! Kuna rafiki yangu tuliongea na yeye nikajaribu kumwambia tulikosana na bibi nikamwambia aende asikie chenye anasema. Alimwambia ati hatukukosana na yeye ilikuwa matatizo ya mawasiliano tu. Kila nikimpigia simu anasema ako na kazi. Kama anasikiza ningependa nimwambie bado nampenda na ikiwezekana akuje nyumbani tuongee. Kama kuna shida yoyote akuje tutaongea na tuendelee kulea mtoto wetu. Kama ameamua kujipanga na maisha yake basi akuwe wazi aniambie nami nijipange" Alisema

Juhudi za kumfikia Bi Jackline ziligonga mwamba kwani alikuwa amezima simu yake.