Patanisho: "Nilikuwa mwizi lakini niliacha, nilikuwa namchapa!" Jamaa akiri alivyokosea mkewe

Muhtasari

•Alikiri kwamba kuna wakati alikuwa jambazi na alikuwa na mazoea ya kumchapa mkewe mara kwa mara, matendo ambayo yalichangia kutengana kwao.

•Maureen alifichua kwamba walipokuwa kwa ndoa John hakuwa mwaminifu na alikuwa na mazoea ya kumchapa mara kwa mara.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama John Kahara (26)  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Maureen (21) ambaye waliachana kufuatia mizozo ya kinyumbani.

John alisema alimuoa Maureen takriban miaka mitano iliyopita akiwa na umri mdogo wa miaka 16 baada ya kumpachika ujauzito.

Alikiri kwamba kuna wakati alikuwa jambazi na alikuwa na mazoea ya kumchapa mkewe mara kwa mara, matendo ambayo yalichangia kutengana kwao.

"Tulipata mtoto na yeye nikaona ni heri nimuoe badala ya kumtupa ama kujificha. Niliona ni heri tuanze maisha mambo iendelee tu. Nilikuwa nafanya kazi pahali. Ameamua kuniacha akaenda kufanya kazi zake Nakuru. Niko na makosa ya kumchapa. Aliniambia anataka kulipiza kisasi. Sikuwa mzuri hapo kitambo, nilikuwa namkosea sana. Nilikuwa mwizi lakini niliacha. Nilikuwa napatikana kwa mambo ya nje. Alitaka kujilipishia atosheke pia. Nilipata mambo zingine kwa simu akaniambia anataka kujilipizia. Kukawa na vita na akachukua vitu vyake akaenda" John alisema.

Maureen alipopigiwa simu alisema tayari amekubali kumsamehe John ila akasisitiza kwamba hakuna uwezekano wa kurudiana.

Maureen alifichua kwamba walipokuwa kwa ndoa John hakuwa mwaminifu na alikuwa na mazoea ya kumchapa mara kwa mara.

"Kukusamehe nilikusamehe lakini hatuwezi rudiana na wewe... ata uko na nguvu za kusema ulikuwa unanichapa. Kama sasa hutaweza kuoa mwingine ambaye utakuwa unachapa, nunua drum uwe unaichapa. Hakuna siku tutarudiana na wewe na usiwahi kutarajia" Maureen alimwambia John.

"Aliishi kunichapa, alikuwa anacheat!" Alisema.

Maureen aliomba kuruhusiwa kuchukua watoto kutoka kwa mume huyo wake wa zamani, jambo ambalo John alikataa na kusisitiza angelea mwenyewe.