Jamaa apost picha na mwanamke mwingine na kuandika 'sipangwingwi' punde baada ya kufukuza mkewe

Muhtasari

•Wangui alieleza kwamba mumewe alimshuku kuwa na uhusiano wa kimapenzi na jamaa fulani aliyekuwa rafikiye ndiposa akamfukuza.

•Alisema kwamba punde baada ya mumewe kumfukuza alipakia picha mtandaoni akiwa na mwanamke mwingine.

•Sylvanus alifichua kwamba Wangui aliwahi kugura ndoa yao kwa kipindi cha mwaka mmoja na wakati aliporudi alikuwa amebadilika sana na hata alimnyima haki zake za ndoa.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha 'Gidi na Ghost asubuhi' kitengo cha Patanisho mwanadada aliyejitambulisha kama Evelyn Wangui kutoka Vihiga alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Sylvanus.

Wangui alisema ndoa yake ilisambaratika baada ya mumewe kumshtumu kwa kutembea nje ya ndoa.

Alieleza kwamba mumewe alimshuku kuwa na uhusiano wa kimapenzi na jamaa fulani aliyekuwa rafikiye ndiposa akamfukuza.

"Kuna huyu jamaa alisoma naye. Huwa namuita baba. Alianza kunishuku kwamba naenda naye na eti alikuwa ananitumia pesa. Bibi yake alikuja akaniuliza kama niko na mahusiano na mumewe. Baadae bibi ya huyo jamaa akapigia mzee wangu simu ndio akaniuliza nikamwambia hakuna kitu kati yetu. Yeye hakutaka kunielewa, alitaka kusikiliza wengine" Wangui alisimulia.

Wangui alikiri kwamba jamaa ambaye mumewe alishuku kuwa kipenzi chake cha siri alikuwa amempatia msaada wa kifedha ili aweze kukidhi mahitaji yake. Hata hivyo alipuuzilia mbali mahusiano kati yao.

Alisema kwamba punde baada ya mumewe kumfukuza alipakia picha mtandaoni akiwa na mwanamke mwingine.

"Alipakia picha yake akiwa na mwanamke mwingine alafu akaandika mimi 'sipangwingwi'... Hiyo siku tu tarehe 30 baada ya dadake kuja kuninyang'anya mtoto ndio alipakia picha  akiwa na mwanamke mwingine. Alikuwa amemshika kwa mabega.. Niliambiwa nifungue simu nione chenye bwanangu amepakia. Kuona vile niliamua kutoka" Alisema.

Sylvanus alipopigiwa simu alisisitiza kwamba Wangui alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na rafiki yake ndiposa akamtema.

Alisema kwamba mkewe na rafiki yake walibadilishana namba za simu kisiri na wakaanza kutumiana jumbe za mapenzi.

"Alichosema kuhusu picha sio kweli. Nimejitolea sana juu yake. Ilikuwa mwezi wa nane mwaka uliopita nilikuwa naenda nyumbani kujenga nikamwambia anilindie vitu vyangu  na mimi nipambane nione vile tutaweza kukimu mahitaji yetu na watoto. Tulijenga nikamuacha nyumbani kisha nikarudi Nairobi. Kuna rafiki yangu tulikuwa tunasoma naye, tulikuwa naye nyumbani wakati nilikuwa najenga. Kumbe kuacha kijana nyumbani walichukuana namba na bibi yangu wakaanza kutumiana jumbe. Ilibidi nimetafuta nauli nirudi nyumbani ili nisuluhishe maneno hayo nikapata ni kweli. Huyo kijana alikuja Nairobi nikamuita kwangu. Kuchukua simu yake nikaona jina na picha ya bibi yangu. Niliona jumbe walizokuwa wametumiana. Walikuwa wanachat WhatsApp" Sylvanus alisimulia.

Alisema kwamba Wangui pamoja na rafiki yake walikana mahusiano yoyote ya kimapenzi kati yao wakati alipowauliza.

Sylvanus alifichua kwamba Wangui aliwahi kugura ndoa yao kwa kipindi cha mwaka mmoja na wakati aliporudi alikuwa amebadilika sana na hata alimnyima haki zake za ndoa.

Wangui alimuomba mumewe akubali kumsamehe na amruhusu aweze kuona na kuwasiliana na mtoto wao.

Sylvanus alisisitiza kwamba hawezi kumruhusu Wangui achukue ama kuwasiliana na mtoto wao.