Patanisho: Jamaa akosana na dadake mkubwa kwa kumuibia TV na Woofer

Muhtasari

•Joseph alikiri kwamba walikosana na dadake baada yake kuiba runinga na radio kutoka kwa nyumba yake mnamo mwezi Mei mwaka jana.

•Lydia alisema kwamba tayari alikuwa amemsamehe nduguye ila akadai  hayuko tayari kumkaribisha tena maishani mwake.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Joseph Kutusi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na dadake Lydia Wakama ambaye walikosana mwaka uliopita.

Joseph alikiri kwamba walikosana na dadake baada yake kuiba runinga na radio kutoka kwa nyumba yake mnamo mwezi Mei mwaka jana.

Alidai kwamba alishawishiwa na bwana ya dadake mwingine kutekeleza kitendo hicho ambacho kiliharibu uhusiano wake na dadake.

"Mume wa dada yangu mwingine alinidanganya niibe alafu mimi nikafanya hivo. Walikuwa majirani. Yeye ndiye aliniabia niibe. Nilipoiba nikajulikana. Kutoka siku hiyo mpaka saa hii hatujawahi kuongea na dadangu. Ameishi kunikasirikia " Alisimulia.

Joseph alieleza kwamba baada ya kufanikiwa kuiba vitu hivyo vya dada yake alivibeba na kuvipeleka mahali ambako vilikutwa.

Alisema kwamba jamaa ambaye alimshawishi kuiba aliachana na dadake na kutoroka baada ya tukio hilo kutokea.

Lydia alipopigiwa simu alisema kwamba alisikitishwa sana na kitendo cha ndugu huyo wake mdogo. 

Alisema uhusiano wao wa ndugu na dada pamoja na heshima ambayo alikuwa amempatia hapo awali zilishuka baada ya tukio hilo.

"Mbona uliamua kunitendea hivo alafu saa hii ndiyo unaenda kwa radio Jambo. Unatarajia sasa tutakaa vipi kama ndugu na dada. Ile heshima ambayo nilikuwa nimekupatia itadumu kweli? Saa hii mahali unaishi hiyo mambo inaendelea bado. Unataka tubaki bila ndugu?  Nini ilifanya ukafika kuniibia? Tulikupatia heshima sisi kama dada zako, mbona uliamua kunitendea hivo" Lydia alimtetesha Joseph.

Mwanadada huyo alisema kwamba tayari alikuwa amemsamehe nduguye ila akadai  hayuko tayari kumkaribisha tena maishani mwake.

Joseph alimuahidi dada yake kwamba atabadilika huku akimhakikishia kuhusu upendo mkubwa ambao anao kwake.

Lydia alimwomba kakake waweze kusaidia baba yao na kumhakikishia kuwa kwa sasa hana kinyongo chochote dhidi yake.