Patanisho: Ndoa yasambaratika baada ya jamaa kuagizwa na kanisa lake aache mkewe

Muhtasari

• Baada ya Samson kushauriwa aache mkewe alitaka kuchukua mali yake yote kwa nyumba na kuondoka ila Lilian akachukua hatua hiyo kabla yake.

• Lilian alieleza  kuwa mumewe aliwahi kumfichulia kuwa ana mtoto mwingine nje ya ndoa ambaye alitaka kuwajibikia.

Image: PATANISHO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho mwanadada aliyejitambulisha kama Lilian alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Bw Samson ambaye walitengana baada ya kutofautiana kidogo.

Lilian alisema aliamua kugura ndoa yake baada ya mumewe kujiunga na kanisa moja ambako alishauriwa kumwacha kwa sababu zisizojulikana.

Baada ya Samson kushauriwa aache mkewe alitaka kuchukua mali yake yote ya nyumba na kuondoka ila Lilian akachukua hatua hiyo mbele yake.

"Alinipigia simu akaniambia kwamba alikuwa ameenda kanisa lingine akaambiwa asirudi kwangu. Sijajua mbona? Nilipouliza aliniambia stori nyingi ambazo hazikunifurahisha. Baadae aliniambia kwamba anakujia vitu vyake. Nilibeba hizo vitu nikaenda nazo. Aliporudi kwa nyumba alipata kama nishaondoka. Jambo hilo lilimasirisha zaidi. " Lilian alisimulia.

Lilian alisema kwamba alifanya maamuzi ya kubeba mali yao ya nyumba na kuenda nayo kwa dadake ili kumzuia mumewe dhidi ya kuichukua.

Alieleza kwamba hakuelewa kilichomfanya mumewe abadilike ghafla baada yao kuwa katika mahusiano mema kwa muda. Hata hivyo alisema kuwa mumewe aliwahi kumfichulia kuwa ana mtoto mwingine nje ya ndoa na alitaka kumwajibikia.

"Kuna wakati aliniambia kuwa ako na mtoto ambaye alizaa nje. Alisema kwamba anashughulika kutafuta karo ya mtoto huyo kwa kuwa eti alikuwa amekaa mihula miwili bila kusoma. Baadae alisema anataka kutafuta nyumba yake mwenyewe akae pekee yake ili asomeshe watoto" Alisema.

Lilian pia alifichua kuwa mumewe hakupendezwa na hali yake ya kuwa mwenye maneno mengi, jambo ambalo alisema huenda lilichangia kutengana kwao.

Juhudi za kumfikia Samson hazikufua dafu kwa kuwa simu yake ilikuwa imezimwa.

Lilian alisema kwamba hawajakuwa wakiwasiliana hivi karibuni huku akidai kuwa Samson amemuweka kwa blacklist. Hata hivyo alisema angependa warudiane kwa kuwa anampenda sana