Tunatarajia maombi ya Patanisho kuongezeka baada ya Valentines- Gidi Ogidi

Muhtasari

•Gidi aliwashauri wanandoa kuangazia mabadiliko ya tabia za wapenzi wao ili kutathmini  iwapo wanapanga kuwaondoa kwenye mipango yao ya Valentines.

•Gidi ametoa hakikisho kwamba ako tayari kusaidia kuwapatanisha wanandoa watakaotofautiana siku hii ya wapendanao.

Image: PATANISHO

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, Gidi Ogidi amedai kwamba anatarajia jumbe za maombi ya Patanisho kuongezeka baada ya siku ya Valentines.

Akizungumza katika kipindi cha asubuhi ya Valentines, Gidi alisema kwamba kuna uwezekano mkubwa wa wanandoa wengi kutofautiana katika msimu huu wa mapenzi. 

"Tunatarajia jumbe za Patanisho kuongezeka baada ya siku hii kupita. Mambo haya hutokea mara nyingi"  Gidi alisema.

Gidi amewashauri wanandoa kuangazia mabadiliko ya tabia za wapenzi wao ili kutathmini  iwapo wanapanga kuwaondoa kwenye mipango yao ya Valentines.

Mtangazaji huyo amesema kwamba msimu huu wa Valentines ndio wakati murwa wa kutathmini iwapo mpenzi wako anakuthamini.

"Huu ndio wakati wa kujua iwapo mpenzi wako anakuthamini. Ukiona mwanaume ameanza kununua asubuhi na ukimuuliza anaanza kuteta kuhusu uchumi, jua anataka kuhepa Valentines," Alisema.

Gidi amedai kwamba katika siku hii maalum kwa wapendanao, mara nyingi watu hutunga uongo tofauti katika juhudi za kuikwepa. 

Suala hili huenda likatia doa katika ndoa nyingi. Gidi hata ametoa hakikisho kwamba ako tayari kusaidia kuwapatanisha wanandoa watakaokosana.