Patanisho: Jamaa aachwa kwa kutumia mkewe mjamzito Sh3 badala ya Sh3000 alizoahidi

Muhtasari

•Jacob alisema hatua yake kutumia mkewe shilingi tatu badala ya elfu tatu alizoahidi ni kwa kuwa alitaka kubaini iwapo ni kweli alikuwa mjamzito.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Jacob Ouma (25)  alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Ruth Nanzala (23) ambaye waliachana naye mwaka jana.

Jacob alisema mkewe aligura ndoa mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita baada ya kumshutumu kwa kukosa kumsaidia kifedha.

"Nilienda kazi ya ukulima. Katika kazi yetu ya ukulima unaweza kupata ama ukose. Niliporudi nyumbani mke wangu aliniomba pesa nikamwambia tutalipwa jioni. Hapo tukaanza kuvurugana. Hakutaka kusikia. Baada ya hapo alipanga vitu vyake akaenda. Aliniweka kwa blacklist," Jacob alisimulia.

Jacob alisema muda baada ya mkewe kuenda kwao alimfahamisha kuwa amebeba ujauzito wake na kumtaka atume pesa. 

Aliahidi kutuma shilingi elfu tatu ila akatuma shilingi tatu pekee, jambo ambalo lilimkera zaidi mkewe.

"Nilimpigia simu akanidanganya ako na mimba . Nilimwambia anielezee ukweli akakataa na kusema nitume pesa. Alisema mimba ni yangu. Nilimdanganya ati nitamtumia elfu tatu kwa simu ila nikatuma shilingi tatu. Sikuwa naamini ako na mimba. Niliambia jirani aende anihakikishie kuwa ni mjamzito," 

Jacob alisema hatua yake kutumia mkewe shilingi tatu badala ya elfu tatu alizoahidi ni kwa kuwa alitaka kubaini iwapo ni kweli alikuwa mjamzito.

Juhudi za kuwapatanisha wanandoa hao ziligonga mwamba kwani Ruth hakupatikana kwa simu.