Patanisho: Baba akiri kumlaani mwanawe asiwahi kupata mtoto

Muhtasari

•Erick alifichua kuwa mzozo ulichimbuka baada yake kuegemea upande wa mamake na kuacha kama amemtusi babake.

•Babake Erick lisema kuwa alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya mwanawe kumtusi na kumkosea heshima.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Erick Mutiga ,26, kutoka Meru alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba yake Julius Kaibuga ambaye walikosana mwaka wa 2013.

Erick alifichua kuwa mzozo ulichimbuka baada yake kuegemea upande wa mamake na kuacha kama amemtusi babake.

Alisema kuwa babake alikasirika na kumlaani kuwa hatawahi kupata watoto maishani, jambo ambalo sasa limekuja kutimia. Alifichua kuwa juhudi zake kupata watoto zimekuwa zikigonga mwamba kwani mara ambazo amejaribu na wanadada tofauti, ujauzito wao umekuwa ukiharibika.

"Nilikosana na babangu 2013 kwa sababu ya mambo ya boma. Aliona ni kama naegemea upande wa mama kisha akanilaani eti sitawahi kupata mtoto. Sasa nimejaribu kupata watoto na wanawake wawili ila kila nikijaribu ujauzito unaharibika. Mke wangu wa pili alienda kwa Nabii akamwambia kuwa nimelaaniwa na babangu. Hakuwa anajua hadithi hiyo ya kwetu.

Hiyo kitu ni uchungu sana. Saa hii watoto wangu wametoka wawili. Nahisi uchungu ndani ya roho. Naona tu ni hayo mambo ya mzee. Huwa nashindwa nitaambia watu namna gani naikanyangia tu kwa roho. Inanisumbua sana," Erick alisema.

Erick alisema anajuta sana kuwahi kumkosea babake na angependa amani ipatikane baina yao kwa kuwa ameshindwa kabisa kuendeleza kizazi.

Babake Erick alipopigiwa simu alikiri kuwa kweli alimlaani mwanawe. Alisema kuwa alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya mwanawe kumtusi na kumkosea heshima.

Bw Julius hata hivyo alikubali kushiriki kikao na mwanawe na kuzungumzia mzozo wao ili aweze kumuondolea laana.

"Ndio, nilimlaani. Hatawahi pata watoto. Akuje tuongee naye kwanza.. yeye ndiye alinitusi. Ukitusi mzazi lazima upatwe na laana," Bw Julius alisema.

Erick alikubali kushiriki kikao na babake na kumhakikishia  kuwa anampenda sana.