Patanisho: Mama mkwe amshtumu jamaa kwa kuwa na mazingaombwe na kumtesa bintiye

Muhtasari

•Mutegi alifichua kwamba ndoa yake ya mwaka mmoja ilisambaratika baada yake kutofautiana na mama mkwe.

•Mutegi alisema mkewe alighadhabishwa na matusi aliyotupia mama yake na akagura ndoa akiwa mjamzito.

Gidi na Ghost asubuhi
Gidi na Ghost asubuhi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, Jamaa aliyejitambulisha kama Kenfrey Mutegi (23) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Purity Gakii (24) ambaye walitengana naye takriban miezi minne iliyopita.

Mutegi alifichua kwamba ndoa yake ya mwaka mmoja ilisambaratika baada yake kutofautiana na mama mkwe.

Alisema mama mkwewe alikuwa anaeneza uvumi kuwa amekumbwa na mazingaombwe na eti anamtesa bintiye, jambo ambalo lilimkera hadi akafikia kumtusi.

"Kuna stori niliambiwa na mamangu vile mama mkwe alikuwa anadai eti mimi niko na majini na natesa mtoto wake. Niliambia bibi yangu aende aambie mama yake aache ujinga na nikamtishia kuwa akiendelea nitamchapa. Ni ile tu nilikuwa na hasira," Mutegi alisimulia.

Alisema mkewe alighadhabishwa na matusi aliyotupia mama yake na akagura ndoa akiwa mjamzito. Mutegi alisema amekuwa akijaribu kumshawishi mkewe arudi ila hajaweza kufanikiwa.

Baada ya majaribio kadhaa ya kumpata Purity hatimaye aliweza kuchukua simu na kukubali kumsikiliza mumewe. Purity alisema tayari amemsamehe mumewe na kumhakikishia kuwa bado anampenda.

"Mimi nishakusamehea. Nimekubali turudiane," Purity alisema.

Wawili hao walikubaliana kupatana baada ya Patanisho ili kujadiliana zaidi kuhusu jinsi ya kuendeleza mahusiano yao.