Patanisho: Jamaa ablock mpango wake wa kando baada ya kumkopa Sh700

Muhtasari

•Esther alisema masaibu yalianza kukumba mahusiano yao ya miaka mitano baada ya Omollo kuomba Ksh 700 kutoka kwake kisha kudinda kuzirejesha.

•Alidai mpenziwe alimfungukia kuhusu mke wake baada yake kukumbwa na ndoto akipigana na mwanamke.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Mwanadada aliyejitambulisha kama Esther Kavete (27) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na baba ya mtoto wake, Geoffrey Omollo (32)  ambaye walikosana naye takriban miezi miwili iliyopita.

Esther alisema masaibu yalianza kukumba mahusiano yao ya miaka mitano baada ya Omollo kuomba Ksh 700 kutoka kwake kisha kudinda kuzirejesha.

Alisema alikasirika kutokana na hayo na kumtupia mpenzi huyo wake cheche za maneno. Baadae mpenzi huyo wake alimblock na hajaweza kumfikia tena.

"Mwezi Februari aliniambia amekosana na bibi mwenzangu. Aliniambia nimtumie pesa arudishe keshoye. Nilienda nikakopa pesa. Nilimtumia Sh700 akaniambia atanipigia kesho yake. Aliniambia angekuja Jumamosi ya wiki hiyo. Ilipofika Jumamosi akazima simu na sikuwezi kumpata tena," Esther alisema.

Esther alikiri kwamba alikua mke wa pili wa Omollo. Alisema anamfahamu mke wa kwanza wa mpenziwe ingawa hajawahi kupata nafasi ya kukutana naye.

Alidai mpenziwe alimfungukia kuhusu mke wake baada yake kukumbwa na ndoto akipigana na mwanamke.

"Niko na mtoto wake. Alikuwa anakuja anakaa mwezi moja ama miwili. Sijawahi kupatana na mke wake wa pili lakini namjua. Shangazi yake ananijua," Alisema.

"Nilikuwa naota nikipigana na mtu nashindwa ni nani. Nilikaa nikamuuliza huyo ni nani. Aliniambia kwa kweli ako na bibi,"

Omollo alipopigiwa simu alipokea ila akakata mara moja punde baada ya kufahamishwa kuwa  Esther ndiye alikuwa anamtafuta.

Esther alisisitiza kwamba bado anampenda Omollo na kumwomba amrudie ili walee mtoto wao pamoja.