Patanisho: Jamaa amwambia mkewe amepata mwanamke mwingine wa kumuosha baada ya kuachwa

Muhtasari

•Chris alifichua kuwa mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili mwezi Machi 2021 wakati alipopoteza kazi yake ya ulinzi na kushindwa kukidhi mahitaji ya familia.

•Mama Janerix alifichua kuwa Chris amekuwa akimtumia binti yake jumbe za matusi na hajakuwa akishughulikia mtoto wao.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Chris Makokha alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Janerix ambaye walikosana naye mwaka jana.

Chris alifichua kuwa mkewe aligura ndoa yao ya miaka miwili mwezi Machi 2021 wakati alipopoteza kazi yake ya ulinzi na kushindwa kukidhi mahitaji ya familia.

"Nilikuwa na kazi ya security ikaisha hapo mwezi wa tatu. Nilipokuwa katika harakati ya kutafuta kazi nyingine nilipata alishatoroka," Chris alisema.

Nimejaribu kuongea na wazazi lakini wananiambia niongee na mke wangu. Nikipigia mke wangu ananiambia niongee na wazazi. Wananipiga chenga tu," Alisema.

Chris aliweka wazi kuwa tayari amepata kazi nyingine na kudai kuwa yupo na uwezo wa kushughulikia familia yake.

Juhudi za kumfikia Janerix ziligonga mwamba. Hata hivyo Gidi aliweza kuwasiliana na mamake Janerix ambaye alifichua ujeuri wa Chris.

Mamake Janerix alifichua kuwa Chris aliwahi kuomba kupatanishwa tena ila hakupiga hatua ya kuenda kwa wakwe wake kama alivyoelekezwa. 

"Wewe hujachukua jukumu la kuja. Umerudi huko tu Radio Jambo. Unawasambua tu bure. Ni ujanja unafanya. Kama ulishindwa kuja nyumbani wacha mtoto atakuwa mkubwa utamuonea kwa TV," Mama Janerix alimwambia Chris.

Chris alijitetea kwa kudai kuwa wazazi wake waliahidi kutangulia kuenda kwa kina Janerix ila hawakufanya vile.

"Ni uwongo mtupu tu anaongea kwa Radio. Vile tuliongea wakati huo mwingine hakuja. Anataka tu asikike kwa TV. Huwa ananitusi," Mama Janerix alisema.

Pia alifichua kuwa Chris amekuwa akimtumia binti yake jumbe za matusi na hajakuwa akishughulikia mtoto wao.

"Hata kuwa hashughulikii mtoto ata siku moja. Mtoto utamuonea kwa TV. Huwa anatumia msichana simu akimwambia eti alipata mtu wa kumuosha," Alisema.

Gidi alimpiga marufuku jamaa huyo kutuma jumbe za Patanisho kwa kuwa hakufuata maagizo aliyopatiwa.