Patanisho: Mwanadada atemwa baada ya mumewe kumfumania na jamaa mwingine kitandani

Muhtasari

•Jerono alisema ndoa yake ilisambaratikana Desemba mwaka jana baada ya mumewe kumfumania na jamaa mwingine kitandani.

•Sharon alisema mumewe alipowafumania alikataa kumpatia nafasi ya kujitetea na badala yake akaanza kumpiga.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi mwanadada aliyejitambulisha kama Sharon Jerono alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe Nickson ambaye walitengana naye miezi mitano iliyopita.

Jerono alisema ndoa yake ilisambaratikana Desemba mwaka jana baada ya mumewe kumfumania na jamaa mwingine kitandani.

"Kuna kijana alikuwa anakuja kwangu. Mume wangu akienda kazini, alikuwa anakuja kukaa na mimi. Jirani yetu alimwambia mume wangu kuwa kuna kijana ambaye huja kwake," Sharon alisimulia.

Mwanadada huyo alifichua kuwa mumewe alimpata akiwa ameketi na jamaa huyo kwenye kitanda chao cha ndoa.

"Alitupa tukicharge simu kama tumekalia kitanda chake. Kijana huyo ni rafiki yangu. Hatukuwa na mahusiano naye," Alisema.

Sharon alisema mumewe alipowafumania alikataa kumpatia nafasi ya kujitetea na badala yake akaanza kumpiga.

"Nampenda sana mume wangu, sitaki kumpoteza. Sijui yule kijana ako wapi kwa sababu ata huwa hanipigii simu," Alisema.

Kwa bahati mbaya, jitihada za Gidi kuwapatanisha wawili hao ziliangulia patupu kwani Patanisho hiyo ilikumbwa na tatizo la mawasiliano.

Wawili hao wana mtoto mmoja pamoja ambaye kwa sasa anakaa na Sharon nyumbani kwao baada ya ndoa yao kugonga ukuta.