Patanisho: Mwanadada agura ndoa ya miaka 10 kisha kuolewa na mpwa wa mumewe

Muhtasari

•Onyango alisema alimfukuza mkewe baada ya kugundua alikuwa anapigiwa simu nyingi tatanishi mida ya usiku.

•Onyango alisema mkewe aliondoka na watoto wao wawili na kumwachia mmoja ambaye anaishi na ulemavu.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Jacob Onyango alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Nancy Auma ambaye walitengana naye takriban miezi miwili iliyopita.

Onyango alisema alimfukuza mkewe baada ya kugundua alikuwa anapigiwa simu nyingi tatanishi mida ya usiku.

Alisema alihofia ndoa yao ya miaka kumi ingeporomoka tena kwa kuwa tukio kama hilo liliwahi kujitokeza tena ambapo mkewe aligura na kuolewa na jamaa aliyekuwa anawasiliana naye.

"Miaka ya hapo awali kabla ya kukosana kuna simu zilikuwa zinaleta shida. Nilipata kuna mtu alikuwa anampigia simu usiku. Akipigiwa alikuwa anatoka nje anaenda kupokea akiwa huko. Mara zingine alikuwa anaweka chakula chini  anatuacha tukila na watoto kisha anatoka nje kupokea simu. Siku moja nilimfuata nikamkuta nje ya ploti akiongea kwa simu. Nikachukua  namba ambayo ilikuwa inampigia ili kufanya uchunguzi. Niligundua kuwa ni mtu ambaye najua kabisa. Nilipata ni kijana ya ndugu wangu wa kambo," Onyango alisimulia.

Alifichua kuwa baada ya kugundua uhusiano wa mkewe na mpwa wake alimfukuza akaenda kuolewa naye. Tukio hilo lilizua uhusiano mbaya kati yake na familia ya nduguye.

"Alitoka wakaenda kuishi naye miezi minane. Nilimtoa kwangu wakaenda kuoana na kijana huyo. Familia yangu ilikosana na wazazi wa kijana. Familia zetu zilishiriki mazungumzo kisha Nancy akakubali kuachana naye. Walipoachana alikuja akaniomba msamaha na nikamsamehe tukarudiana"

"Kutoka turudiane imekuwa miaka miwili sasa. Alianza kupigiwa zile tena. Akifika kwa nyumba alikuwa anaweka simu yake flight mode. Usiku moja alienda bafu nikachukua simu yake nikapata missed calls tano. Nikapata kila siku hiyo namba hupiga. Sikujua ni ya nani. Nilipomuuliza ni nani hakuniambia ni nani. Tukaongea na tukaombana msamaha. Hiyo namba ikaendelea kupiga. Siku moja nikampata kwa ngazi akiongea. Alizungumza kwa saa moja tukagombana nikamwambia aende," Alisimulia Onyango.

Onyango alisema mkewe aliondoka na watoto wao wawili na kumwachia mmoja ambaye anaishi na ulemavu.

Nancy alikataa kupatana na Onyango na kukata simu punde Ghost alipowapatia fursa ya kuzungumza.

Onyango alisema takriban wiki mbili zilizopta mkewe alimwambia kuwa hataki kuwa anamkosea tena. Pia alimwambia kuwa anaogopa kurudiana naye kwa kuwa anahofia maisha yake kutokana na hasira zake.