Patanisho: Mwanadada agura ndoa baada ya mumewe kuenda kulewa na kumuacha akiugua

Muhtasari

•Eric alisema ndoa yake ya miaka minne ilisambaratika takriban mwezi mmoja uliopita baada yake kuenda ulevini na kumuacha Ruth akiwa mgonjwa.

•Ruth alilaamikia hatua ya mumewe kumuacha nyumbani akiwa mgonjwa na kutokana na hayo akasita kurudia kwake.

Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Ghost Mulee na Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Eric Mwiti alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Ruth Mwendwa.

Eric alisema ndoa yake ya miaka minne ilisambaratika takriban mwezi mmoja uliopita baada yake kuenda ulevini na kumuacha Ruth akiwa mgonjwa.

"Mimi ata sikujua eti tulikosana. Aligonjeka nikarudi nyumbani nikiwa mlevi nikapata akiwa anawekwa kwa gari apelekwe hospitalini... Nilikuwa najua ni mgonjwa kwa sababu nilirudi nyumbani Ijumaa. Jumamosi hali yake ikawa mbaya nikapatwa na msongo wa mawazo nikaona niende nikunywe kidogo kupunguza," Eric alisema.

Eric alisema baada ya mkewe kutibiwa na kuruhusiwa kutoka hospitalini aligura nyumbani na kuenda kuishi na dadake.

Ruth alilaamikia hatua ya mumewe kumuacha nyumbani akiwa mgonjwa na kutokana na hayo akasita kurudia kwake.

"Nimekuwa nikijaribu kuongea na yeye lakini ata ameniblock. Anataka nimpatie saluni yake na nimgawie mali kidogo aende akaishi Meru," Alisema.

Ruth alipopigiwa simu alikataa katakata kuzungumza na Eric. Alisema kwamba ingawa tayari amemsamehe hayupo tayari kurudiana naye.

"Mwambie sitaki aniombe msamaha kabisa. Nilimsamehe kitambo lakini stori zake sitaki kabisa," Ruth alisema.

Eric alipoulizwa kama amewahi kumkosea mkewe tena alisema ,"Kuna wakati sikuwa na pesa ya kununua mkate tukakosana. Wakati mwingine alinikuta nikihanya msichana mwingine lakini nilimthibitishia kuwa sio mimi ni huyo mwanamke ambaye alikuwa ananitaka."

Alisema kuwa kwa sasa moyo wake unauma sana na angetamani Ruth akubali kumsamehe na warudiane.

"Ruth nakuomba tafadhali unisamehe, Sitaki muwe mbali na mimi. Vile nilikukosea sitawahi kurudia. Wewe na mtoto wangu ndio maisha yangu," Alisema.