Patanisho: Jamaa amfukuza mkewe kwa kuuza kuku wake akiwa kazini

Brian alidai kuwa mamake Mercyline alimtupia cheche za maneno baada yao kutengana

Muhtasari

•Mercyline alisema mumewe alimfukuza kufuatia madai ya kuuza kuku wake bila idhini.

•Brian pia alidai kuwa mamake Mercyline alimtupia cheche za maneno baada yao kutengana.

Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho Mercyline Ayieko alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Brian Okemwa.

Wawili hao walitengana mwezi Aprili mwaka huu kutokana na fitina za majirani na ukosefu wa amani nyumbani, kulingana na ujumbe wa Mercyline.

Mercyline alisema mumewe alimfukuza kufuatia madai ya kuuza kuku wake bila idhini.  

“Tulikuwa tu tunaishi vizuri. Watu wakaanza kumletea fitina kuwa nauza kuku zake. Lakini kuna mbwa ambaye alikuwa anawakula. Siku moja alimfuata mbwa huyo na akaona ni kweli,” Mercyline alisema.

Mercyline alisema kuwa mumewe alimpatia nauli aende kwao licha ya kuthibitisha kuwa kuna mbwa ambaye alikuwa anawakula kuku wake.

Alisema ati mbwa amekula kuku moja tu hizo zingine ni mimi nauza. Alinipatia nauli akasema angenitumia ya kurudi.

Pia ilifika mahali nyanyake akasema kuwa hata hanitaki pale. Mimi nataka kurejea. Mtoto niko naye,” Mercyline aliongeza.

Ghost alipomfikia Brian  kwa simu alisisitiza kuwa mkewe alikuwa anawauza kuku wake wakati akiwa kazini.

“Kama nimeenda kazi anauza kuku.  Sio mbwa alikuwa anakula.  Atakuja tu. Atarudi baada ya wiki moja hivi,” Brian alisema.

Brian alidai kwamba hata aliwahi kuona mahali mkewe aliwauza kuku wao wawili.

Pia alidai kuwa mamake Mercyline alimtupia cheche za maneno baada yao kutengana miezi mitatu iliyopita.

“Kuna siku alipiga simu na mimi sikuwa karibu. Mama yangu ndio alichukua. Nilisikia ati walitusiana,” Mercyline alieleza.

Aliongezea kuwa “Mama alikuwa na hasira kuhusu vile bwanangu alinifukuza,”

Wawili hao hata hivyo walikubaliana kurudiana na kuhakikishia kuhusu upendo wao kwa kila mmoja.

“Nitamtumia pesa Jumamosi,” Brian alisema.