Patanisho: Jamaa amkata kakake mkubwa baada ya kupewa shamba kubwa

Vincent alikiri kuwa alikuwa amevuta bangi kiasi alipomshambulia kaka yake mkubwa.

Muhtasari

•Vincent alifichua kuwa alimuonea kijicho kaka yake mkubwa baada ya kupewa kipande kikubwa cha shamba na kuchukua hatua ya kumkata na panga.

•David alimwagiza  kaka yake mdogo arejeshe radio ya baba yao ambayo alibeba wakati alipotoroka.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, Vincent Wekesa (20) kutoka Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na kaka yake David (27) aliyekosana naye kufuatia mzozo wa shamba.

Vincent alifichua kuwa alimuonea kijicho kaka yake mkubwa baada ya kupewa kipande kikubwa cha shamba na kuchukua hatua ya kumkata na panga mwezi Desemba mwaka jana.

"Babangu alimpenda ndugu yangu mkubwa sana. Ilipofika wakati wa kugawa shamba akamgawia shamba kubwa, mimi kuona hivo nikachukua panga nikamkata alafu nikahamia Nairobi," Vincent alisema.

Alisema alikasirika baada ya babake kukataa kutatua mzozo kati yake na nduguye akimshtumu kwa kuwa mvivu.

Vincent hata hivyo alisema kuwa sasa anajuta yaliyotokea na kueleza kuwa angependa kurudi nyumbani ili aweze kujenga nyumba.

"Kaka yangu alipona kitambo. Kwa sasa niko kwa dadangu, nafanya kazi kwa nyumba," Alisema.

David alipopigiwa simu alifichua kabla ya kutoroka nduguye mdogo alikuwa kero nyumbani na tishio kwa kila mtu.

"Ilifika wakati akataka kupiga kila mtu kwa boma. Alikuwa anashika panga anaanza kukimbia nayo kila mahali. Sijui ni mapepo alikuwa nayo ama ni bangi alikuwa anavuta," Alisema David.

Hata hivyo aliweka wazi kuwa tayari amemsamehe Vincent na hana shida yoyote naye.

"Mimi sina shida na wewe. Kama ni kukusamehe nilikusamehe kitambo. Lakini saa hii usilete hiyo kichwa yako mbaya," Alisema.

Vincent alitoa hakikisho kuwa kwa sasa tayari amebadilisha mienendo yake na kuomba apokewe vizuri nyumbani.

"Ilikuwa tu mara moja ambapo nilikuwa nimetumia bangi nikaenda kwa boma nikamchapa. Saa hii nimetulia na nimeacha," Alisema.

David hata hivyo alitoa sharti kwa kakake mdogo arejeshe radio ya baba yao ambayo alibeba wakati alipotoroka.

Vincent kwa upande wake aliahidi kurejea nyumbani na radio na TV ambazo tayari amenunua. Pia aliahidi kuendeleza mienendo miema.