Patanisho: Mke amfukuza mwanadada aliyeletwa nyumbani na mumewe na kumpa nauli

Sylvia alisema kuwa ndoa yake ilisambaratika wakati akiwa amebeba ujauzito wa mtoto wa tatu na Bw Francis.

Muhtasari

•Sylvia alidai kuwa mama mkwe wake anamchukia bila sababu na alisababisha kutengana kwake na mumewe mnamo mwezi Juni.

•Baadae Francis alileta mwanamke mwingine wakati na Sylvia kufikiwa na habari hizo akarudi na kukabiliana naye.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Slyvia kutoka Kajiado alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Francis Kipamet ambaye aliachana naye kufuatia mizozo ya kifamilia.

Sylvia alidai kuwa mama mkwe wake anamchukia bila sababu na alisababisha kutengana kwake na mumewe mnamo mwezi Juni.

Alisema kuwa ndoa yake ya miaka minne ilisambaratika wakati akiwa na ujauzito wa mtoto wa tatu na Bw Francis.

"Tulikuwa na mipango ya kujenga. Mama mkwe hakuwa anataka. Alikuwa anataka mwanamke mwingine ajengewe," Sylvia alisimulia.

Alisema kuwa kufuatia mzozo huo alienda nyumbani kwao huku mikakati ya kutafuta suluhu ikiendelea.

Baadae Francis alileta mwanamke mwingine wakati na Sylvia kufikiwa na habari hizo akarudi na kukabiliana naye.

"Nikiwa nyumbani kwetu nilipigiwa simu nikaambiwa jamaa ameleta mwanamke mwingine. Niliporudi  mwanamke huyo aliniambia kuwa aliambiwa hakuna mwanamke mwingine pale. Alisema kuwa yeye ni yatima na hana nauli ya kurudi. Nilimpatia fare akaenda mpaka kwa Muranga," Alisema.

Sylvia alisema baada ya tukio hilo mumewe alipendekeza wahame pale nyumbani na kuenda kukodi nyumba kwingine.

Alisisitiza kuwa hakuwahi kuelewa sababu za mama mkwe wake kumchukia na kudai kuwa kila siku alimheshimu.

Patanisho ya Sylvia na Francis hata hivyo haikuweza kuendelea kutokana na shida za mawasiliano.