Patanisho: Mwanadada afunguka alivyoolewa akiwa na miaka 13 baada ya wazazi kuaga

Atieno alisema mama mkwewe alikuwa akimshtumu kwa uasherati na kuzua ugomvi kati yake na mumewe.

Muhtasari

•Atieno alisema ndoa yao ya miaka minane ilisambaratika Januari mwaka jana kufuatia fitina nyingi za mama mkwe wake.

•Atieno alieleza kuwa wakati alipotoroka aliwaacha watoto wao wanne mikononi mwa mumewe.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi chetu cha Gidi na Ghost asubuhi kitengo cha Patanisho, Joyce Atieno alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mumewe George Okumu.

Atieno alisema ndoa yao ya miaka minane ilisambaratika Januari mwaka jana kufuatia fitina nyingi za mama mkwe wake.

Alisema mama mkwewe alikuwa akimshtumu kwa uasherati na kuzua ugomvi kati yake na mumewe, jambo lililomsukuma kutoroka.

"Bwanangu alikuwa naenda kazi asubuhi, akirudi mama mkwe anamwambia pia mimi nilikuwa nimetoka. Alikuwa anasema niko na usherati. Hata nikienda sokoni alikuwa anasema nimeenda kutafuta wanaume. Hata nikirudi kama nimebeba jembe anasema nimetoka usherati," Atieno alisimulia.

Alisema kuwa mumewe hakuwahi kumuamini kila alipojitetea na badala yake aliyaamini maneno ya mamake.

"Mume wangu alikuwa ananiambia niache kujibizana na mamake.. Kwa sasa niko nyumbani. Nilitoka juu alikuwa ananipiga kabisa. Nataka kurudi juu nilisikia watoto hawako katika hali nzuri," Alisema.

Atieno alieleza kuwa wakati alipotoroka aliwaacha watoto wao wanne mikononi mwa mumewe.

"Naomba anipatie watoto wangu niwalee. Naweza kuwalea vizuri na asikuje kuwatamani baadae. Nilikuwa nataka kuhama na watoto wangu lakini alikataa"

Juhudi za kumpatanisha mwanadada huyo na Okumu hazikufua dafu kwani hakushika simu licha ya Gidi kufanya majaribio kadhaa.

"Huyo ametorokwa na mabibi wengine. Sikuwa bibi wake wa kwanza. Nilipata kama wengine wameshatoroka," Atieno alifichua.

Atieno alifichua kuwa aliolewa akiwa na umri mdogo sana baada ya wazazi wake kuaga na yeye kubaki yatima.

Alieleza kuwa alipata mtoto wake wa kwanza akiwa na umri wa takriban miaka 13.