Patanisho: "Alinishikia kisu mara mbili!" Mwanadada asimulia masaibu ya ndoa yake

Nekesa aligura ndoa yake wakati mumewe alipompiga baada ya kushuku ana mpango wa kando.

Muhtasari

•Kiplangat alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitano wakati alipompiga baada ya kushuku ana mpango wa kando.

•Nekesa alifichua kuwa yeye ndiye alikuwa akigharamia mahitaji ya familia yao baada ya mumewe kukataa kazi aliyokuwa amepata.

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Vincent Kiplangat alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mkewe Pauline Nekesa ambaye alimtema mapema mwaka huu.

Kiplangat alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitano wakati alipompiga baada ya kushuku ana mpango wa kando.

"Kuna mtu alikuwa anaongea na yeye kwa simu. Alikuwa akirudi jioni alafu anatoa line kwa simu. Tulikaakaa kidogo nikajua hayo maneno lakini sikuwahi kumpata," alisema.

Alifichua kuwa jamaa aliyekuwa akimnyemelea mkewe alijileta nyumbani kwake na kuomba msamaha

"Aliniambia hakujua ni mke wa mtu.  Aliniambia hakuna kitu walifanya,"

Kiplangat alisema hakujakuwa na uhusiano mzuri kati yake na mkewe tangu alipogura ndoa yao na kurudi kwao. Pia alifichua kuwa hakuwahi kutembea kwa kina Nekesa hadi wakati walipokuwa pamoja.

"Nimejaribu hata kuambia mama yangu aende lakini nimeambiwa nimbembeleze arudi ndio waende waongee," alisema.

Nekesa alipopigiwa simu alisema mumewe alikuwa akiyasikiliza sana maneno ya watu na kuyaamini. Alisema kuwa wanaume waliokuwa wakimchokoza ni wateja katika hoteli anakofanyia kazi.

Aidha alifichua kuwa Kiplangat ni mwenye vurugu na aliwahi kumtishia kwa kisu mara mbili  walipokuwa pamoja

"Alinishikia kisu mara mbili. Mara ya kwanza nilimsamehe lakini ya pili nikasema niende kwetu mimi bado naweza kurudi shule," alisema.

Alimuuliza mumewe "Unanipiga aje na hata kwetu sijawahi kupigwa?!"

Nekesa pia alifichua kuwa yeye ndiye alikuwa akigharamia mahitaji ya familia yao baada ya mumewe kukataa kazi aliyokuwa amepata.

"Nilikuwa naenda kazi  namuacha kwa nyumba alafu nagharamia kila kitu. Hawezi kuona hilo.  Alikuwa ameenda kazi akakataa akasema ni ngumu," alisema

Kiplangat alijitetea kwa kusema "Mimi huwa na Ashtma na kazi nilikuwa nimepata ni ya moshi,"

Nekesa hata hivyo alikubali msamaha wa mumewe na kumuomba apige hatua ya kufika nyumbani kwao ili waweze kusuluhisha mzozo wao.

Pia alimhakikishia Kiplangat kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kusema yuko tayari kurudi.