Patanisho: Jamaa amtema mkewe baada ya kuzaa mtoto anayefanana na jirani

Nyaboke alikiri kupachikwa ujauzito na jirani woria ambaye alikuwa akiuza miraa.

Muhtasari

•Simon alidai alimkuta mkewe ni mjamzito na mambo hakuelewa ilivyofanyika kwa sababu alikuwa ametoka nyumbani kwa muda. 

•Simon alifichua kwamba alifanya ndoa ya kanisa na Nyaboke mwaka wa 2016.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Simon Nyang'au ,30, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Yunuke Nyaboke ,27, ambaye alitengana naye takriban mwaka mmoja uliopita kufuatia masuala ya kinyumbani.

Simon alisema kuwa mkewe aligura ndoa yao ya miaka mitatu baada ya kumkabili kwa kuzaa na mtoto anayefanana na jirani yao. Alisema kuwa aligundua mtoto wa tatu wa mkewe alifanana na jirani yao mwenye asili ya Kisomali (Woria) mwezi moja tu baada ya kuzaliwa.

"Kuna mambo mengine ambayo yalisababisha mimi kujua. Tulitoka nyumbani Januari mwaka jana, kurudi Nairobi nikapata kazi huko Meru. Lockdown ya Corona ilipokuja nikafungiwa huko Meru. Niliporudi mwezi wa nne ndio niliona maajabu yametendeka na sikufahamu," alisimulia.

Simon alidai kuwa alimkuta mkewe ni mjamzito na mambo hakuelewa ilivyofanyika kwa sababu alikuwa ametoka nyumbani kwa muda. Mwezi mmoja baada ya mtoto kuzaliwa ndipo alipogundua kuwa anafanana na jirani wao ambaye alikuwa akiuza Miraa.

Alisema baada ya kukabiliana na mkewe na kumuuliza kuhusu suala hilo waligombana na baadaye wakaalika wazee na wanafamilia kutafuta suluhu. Nyaboke alikiri kupachikwa mimba na jirani huyo ila wakawa na maafikiano na kukubaliana kuendeleza ndoa.

"Tuliongea na tukakubaliana. Sababu ya aibu alitoroka akaenda. Nilibaki na watoto wawili. Alienda na mmoja," alisema.

Simon alifichua kwamba alifanya ndoa ya kanisa na Nyaboke mwaka wa 2016.

Juhudi za kuwapatanisha wanandoa hao hata hivyo hazikufua dafu kwani Nyaboke alikosa kushika simu.

Simon alipopewa nafasi ya kuzungumza naye hewani alisema, "Makosa hufanyika. Naomba urudi kwa ajili ya watoto wengine ambao tuko nao. Tulizungumza na tukakubaliana. Mimi sina neno. Kubali tu na urudi. Ata kama ni kuhama huku tutahama."