Patanisho: Jamaa amfumania mkewe na fundi wa pikipiki

"Ningependa turudiane naye tulee watoto," alisema.

Muhtasari

•Bernard alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka kumi na miwili baada ya kumfumania na fundi wa pikipiki.

•Beryl alidai kwamba baba mkwe wake aliwahi kumshambulia, tukio ambalo lilifanya atoroke na kurudi kwao.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Bernard Kisali ,32, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Beryl ,27, ambaye alitengana naye  mapema mwaka huu.

Bernard alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka kumi na miwili baada ya kumfumania na fundi wa pikipiki.

"Nilikuwa  naenda kazi asubuhi narudi jioni. Kumbe mke wangu alikuwa na mambo zake. Yule jamaa wa bodaboda nilikuwa napatie vitu alete vitu nyumbani, niliwafumania naye kwa nyumba yake. Nilijaribu kumuuliza akaogopa akaenda kwao," Bernard alisimulia.

Bernard alisema mkewe alitoroka pamoja na watoto wao watatu na hajakuwa akipokea simu zake kila anapochukua hatua ya kupiga.

"Ningependa turudiane naye tulee watoto. Watoto wako naye. Niliwahi kuenda kwao nikakuta hayuko," alisema.

Beryl alipopigiwa simu alikanusha madai mengi yaliyotolewa na mume huyo wake aliyetengana naye. Alidai kwamba Bernard hakuwahi kujitambulisha kwa wazazi wake na hakuwa akiwajibika nyumbani.

"Tangu tuoane hajawahi kujishughulisha kujua kwetu ama kutembelea wazazi wangu. Nilikuwa kwao alafu nikapata kazi Nakuru nikahama. Mimi ata ndio nilimtafutia kazi Nakuru baadae," alisema.

Pia alidai kwamba baba mkwe wake aliwahi kumshambulia, tukio ambalo lilifanya atoroke na kurudi kwao.

"Wakati babake alikuja akanipiga, nilikuwa mjamzito. Nilienda nyumbani nikajifungua mtoto wangu wa tatu. Nilieleza wazazi wangu wakasema hapo hakuna ndoa. Hakuwa akiwajibika mtoto," alisema.

Beryl alisema baada ya kujifungua mtoto wa tatu ndipo alipopata kazi jijini Nakuru na kuhamia huko.

"Nilimtafutia kazi Nakuru akakuja. Baadae alianza kukosa kuwajibikia majukumu ya nyumbani. Nilivumilia tu," alisema.

Aidha, mama huyo wa watoto watatu alikanusha madai ya kutoka kimapenzi na fundi wa pikipiki.

"Yule jamaa wa kutengeneza pikipiki, ni ukweli ama ni uongo?" Bernard alimuuliza.

Beryl alijibu, "Mwanaume yupi ulifumania naye?.. Vile ulitukuta ulichukua jukumu lipi?"

Aliweka wazi kuwa hayupo tayari kurudiana na mzazi huyo mwenzake na kumuomba ashughulikie watoto wao.

"Huwa anasema atatuma pesa, sijawahi kuona kitu. Kama ni kusaidia watoto ni sawa," alisema.

Bernard alimwambia, "Kaa chini, upunguze hasira alafu urudi tuendelee na maisha."