Patanisho:Mwanaume anayeishi mbali na nyumbani ataka hakikisho la upendo kutoka kwa mkewe

Joshua alitaka mkewe kumhakikishia kuwa anampenda

Muhtasari

• Joshua alisema kuwa sababu yake ya kutaka kujua iwapo mkewe anampenda ni kuwa anaishi mbali na mke wake.

Mtangazaji Gidi
Image: Radio Jambo Instagram

Katika kipindi cha Gidi na Ghost, kitengo cha Patanisho, Joshua kutoka Migori alitaka kujua iwapo mke wake, Kerubo anampenda.

Joshua alisema kuwa sababu yake ya kutaka kujua iwapo mkewe anampenda ni kuwa anaishi mbali na mke wake.

"Naishi mbali, mke wangu anaweza kudhani kuwa simpendi. Nataka kujua iwapo ananipenda au ananiamini," Joshua alimwelezea Gidi.

Mke wake alipopigiwa, jamaa huyo alipata nafasi ya kumweleza mke wake jinsi anavyompenda sana.

"Nilipiga Radio Jambo unihakikishie kuwa unanipenda, kwa kuwa niko mbali na niko kazi. Sifanyi mambo mengine, nafanya kazi tu," alisema.

Joshua alimkumbusha mkewe jinsi walivyopitia mengi kwenye ndoa yao ya miaka mitatu na hangetaka lolote liwatenganishe.

"Nimekuchagua kama mke wangu wa maisha, tumetoka mbali , nakupenda sana,"Joshua alizidi kumweleza mkewe.

Mke wake hata hivyo, hakuongea wala kusema chochote kwa mume wake, alikuwa anakubaliana tu na mume wake.

Hata hivyo, jamaa huyo alisema kuwa yeye na mke wake huwasiliana kila siku licha ya kuishi mbali.

Mke wake ndiye anayeishi na watoto wao wawili na anafanya ukulima.

Wasikilizaji hata hivyo walitoa maoni yao ambayo yalibishana na sababu ya Joshua kutaka kujua iwapo mke wake wa miaka mitatu anampenda.

Mwanamke mmoja aliwashauri kuzoea kuwa na mawasiliano kila siku kwani yeye na mume wake pia wamekuwa kwenye hali hiyo.

Joshua alijitetea kwa kusema kuwa yeye huenda kanisani ambapo hufundishwa kuwa na maadili mema kwa hivyo ni mwaminifu.

Baadhi ya wasikilizaji pia walitoa maoni yao:

"Angetulia alivyo, hangesema chochote, mke wake ataanza kumshuku kwani yeye mwenyewe amejishuku sana,"mwanaume mmoja alisema.

"Jambo la kuishi mbali na mwanamke ni jambo hatari sana, usikae mbali sana kwa muda mrefu,hata hivyo kuwa na uzoefu wa kuheshimu ndoa yako".

"Huyo jamaa asilete utoto kwenye redio, angeenda tu nyumbani".

"Huwezi kuishi na mke wako kwa ndoa kama rafiki, siwezi kuuliza mke wangu kama ananipenda kwani ananilelea watoto".

Mtangazaji Gidi
Image: Radio Jambo Instagram
Mtangazaji Gidi
Image: Radio Jambo Instagram