Patanisho: Jamaa ataka kuuza TV akanunue nyama, akataa maharagwe na mboga

"Akikuja anasema anataka nyama. Ananiambia sitaki kula mboga, nataka kula nyama," Janet alisema.

Muhtasari

•Albert alisema mke wake alimtema  mwezi Juni mwaka jana baada ya kuchoshwa na uraibu wake wa pombe.

•Albert hata hivyo alimsihi mkewe arudi huku akimhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake.

Mtangazaji Gidi Ogidi
Image: RADIO JAMBO

Bwana Albert Mogeni alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Janet Kemunto ambaye walikosana naye kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Albert alisema mke wake alimtema  mwezi Juni mwaka jana baada ya kuchoshwa na uraibu wake wa pombe.

"Nimejaribu kumfuatilia lakini sijafanikiwa. Huwa namtumia pesa anasema anakuja alafu ikifika wakati wa kurudi anabadilika. Huwa ananiambia bado ako kwao. Anasema ati mimi nakunywa pombe yake, eti nikiacha atarudi," alisema.

Albert alikiri kwamba kila siku kwa kawaida huwa anabugia chupa mbili za mvinyo.

Janet alipopigiwa  simu aliweka wazi kuwa ni kweli alitoroka kufuatia tabia ya mumewe ya kulewa. Alifichua kuwa kabla ya kufikia hatua ya kugura ndoa yake, Albert alikuwa akidai nyama baada ya kutoka ulevini.

"Akikuja kutoka ulevini anataka nyama. Ananiambia sitaki kula mboga nataka kula nyama," alisema.

Aliongeza, "Siku moja alisema anataka kuuza TV akanunue nyama. Alisema hawezi kula maharagwe. Alinichapa nikaondoka."

Albert alisisitiza kwamba ameanza safari ya kuacha pombe polepole na kudai kuwa anakusudia kuacha kabisa katika siku za usoni.

"Wewe kwanza badilika. Sitaruhusu Janet arudi kama bado unakunywa pombe," Gidi alimshauri Albert.

Albert hata hivyo alimsihi mkewe arudi huku akimhakikishia kuhusu upendo wake mkubwa kwake. 

Janet alisema,"Kwanza acha pombe, kama bado hujaacha siwezi kurudi. Sitakuja kuteseka."