Patanisho:Jamaa ajawa na wasiwasi baada ya mke wake mjamzito kutishia kujitoa uhai

Kipkorir alisema mkewe alianza kulalamika alipogundua ni mjamzito.

Muhtasari

•Kipkorir alisema mkewe ambaye ana ujauzito wa takriban wiki tatu aligura nyumbani hivi majuzi na kudai hajui mahali alipokwenda.

•"Nimejaribu kumfuatilia ata sijui ako wapi. Alitoroka juzi. Tulioana naye 2019 na tuko na mtoto mmoja pamoja," alisema.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Mtangazaji Jacob Ghost Mulee ndani ya studio za Radio Jambo.

Katika kitengo cha Patanisho, Kelvin Kipkorir (25) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Valentine Cheruu (20).

Kipkorir alisema mkewe ambaye ana ujauzito wa takriban wiki tatu aligura nyumbani hivi majuzi na kudai hajui mahali alipokwenda.

Alisema mkewe alianza kulalamika kuhusu msongo wa mawazo pindi alipogundua kwamba ni mjamzito.

"Mke wangu ananisumbua ananiambia ati ako na stress na anataka kutoa mimba. Anasema eti atafukuzwa kwao. Anasema hakuwa anatarajia mimba. Kila wakati huwa ananitishia kuwa atajiua," Kipkorir alisimulia.

"Nimejaribu kumfuatilia ata sijui ako wapi. Alitoroka juzi. Tulioana naye 2019 na tuko na mtoto mmoja pamoja," alisema.

Kipkorir alidokeza kuwa sio mara ya kwanza kwa tabia za mkewe kubadilika akiwa mjamzito huku akieleza kwamba hata alipokuwa amebeba ujauzito wa mtoto wao wa kwanza bado alikuwa akimsumbua.

"Yeye huwa anakasirika  sana hadi unapata amechukua vitu vyake na kuenda.Tulionana naye kwa mara ya mwisho siku ya Jumatatu.Mimba ni ya wiki tatu na ananiambia kuwa inamsumbua atatoa ," alisema.

Juhudi za kuwapatanisha Kipkorir na mkewe hata hivyo hazikufua dafu Ghost hakuweza kumpata Cheruu kwa simu.

Je, ungemshauri Kipkorir vipi?