Patanisho: Jamaa aachwa na mchumba wake siku mbili kabla ya ndoa

Sharon alichumbiana na Brian muda mfupi baada ya kutengana na baba ya mtoto wake.

Muhtasari

•Brian alisema mchumba wake alimtema mwishoni mwa mwezi Desemba baada ya kumshtumu kwa kutumia dawa za kulevya.

•Sharon pia aliibua madai kwamba mpenzi huyo wake wa zamani aliwahi kutaka kumpiga baada ya kuzozana

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost kitengo cha Patanisho, Brian Muganda ,23, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mchumba wake Sharon ,20.

Brian alisema mchumba wake alimtema mwishoni mwa mwezi Desemba baada ya kumshtumu kwa kutumia dawa za kulevya. Wakati huo, wawili hao walikuwa wamepanga kufunga ndoa na kuishi pamoja.

"Tulikuwa tumepanga kuoana tarehe Desemba 24. Msichana mwenyewe alikuwa amezungumza na wazazi wangu. Kufika tarehe 22, nilienda kwake kumuona na kumpatia pesa ambazo alikuwa akitaka. Niliona ako na hasira. Hata pesa ambazo nilikuwa nimpatie sikumpatia," Brian alisimulia.

Brian alisema mipango ya ndoa ambayo walikuwa nayo haikutumia kwani mchumba wake tayari alikuwa amemtema.

"Mnamo Desemba 24 usiku, alinitumia ujumbe akaniambia stori zangu na yeye ziishe. Nilienda kwake baada ya siku mbili nikumuuliza sababu ya kuniacha. Nilipata bado ako na hasira. Alisema nimpatie charger yake na betri," 

Brian alidai alikuwa akimsaidia Sharon tangu walipokutana mwezi Novemba licha ya kuwa na mtoto mmoja kutoka kwa ndoa ya awali.

Sharon alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba hayupo tayari kurudiana na mpenzi huyo wake wa zamani.

Mama huyo wa mtoto mmoja alidai kwamba Brian ni mtumizi wa bangi na ana 'utoto', mambo ambayo hawezani nayo.

"Mimi sipendangi utoto. Alisema eti alituma ujumbe nikakosa kujibu ilhali mimi sikuona. Nilitoka nikienda matanga ya shemeji yangu, Alisema eti aliniona. Nilimwambia kama anataka kunichunga ataumia," alisema.

Sharon pia aliibua madai kwamba mpenzi huyo wake wa zamani aliwahi kutaka kumpiga baada ya kuzozana.

"Ulikuwa umetumia zako ulitaka kunichapa. Siwezi kurudi nyuma tena," alisema.

Sharon alifichua kwamba alijitosa kwenye mahusiano na Brian mnamo Novemba 3, muda mfupi tu baada ya kukatiza mahusiano na baba ya mtoto wake.

"Sikuwa nimekawia nilikuwa nimetoka kwa mwingine. Tulikuwa tumekosana na mume wangu juu ya wanawake," alisema.

Brian alidokeza kuwa sasa yuko tayari kusonga mbele na maisha yake baada ya majaribio nane ya kuomba msamaha kugonga mwamba.