Patanisho: Bashasha huku jamaa akipatana na mkewe mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake

"Haniamini. Ameacha kuniamini kabisa!" Faith alisema.

Muhtasari

•Faith alisema kwamba hakujakuwa na uaminifu katika ndoa ya kwa muda wa kipindi cha siku chache zilizopita.

•Alisema kwamba alilazimika kumtafuta baba mtoto wake kwa kuwa mumewe hakuwa akisaidia katika malezi yake.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Mtangazaji Jacob Ghost Mulee ndani ya studio za Radio Jambo.

Katika kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi, kitengo cha Patanisho, mwanadada aliyejitambulisha kama Faith Abisai (23) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Boniface Mbote (26) ambaye uhusiano wake naye umezorota.

Faith alisema kwamba hakujakuwa na uaminifu katika ndoa ya kwa muda wa kipindi cha siku chache zilizopita baada ya yeye kuwasiliana na baba wa mtoto wake akikusudia kumuomba usaidizi katika  malezi ya mtoto.

"Haniamini. Ameacha kuniamini kabisa!" Faith alisema.

Alifichua kwamba aliingia kwenye ndoa na Boniface akiwa na mtoto mmoja tayari ilhali mumewe alikuwa na watoto wengine wawili kutoka kwa mahusiano ya awali na alikuwa akihusika katika malezi yao.

"Ako na watoto wawili kando. Niko na mtoto mmoja. Akinioa hakuniambia ako na watoto. Mimi nilimwambia ukweli kwamba niko na mtoto mmoja," alisema.

"Wakati nilipata mimba ndipo aliniambia ako na watoto wengine wawili na wanawake tofauti," Faith alisema.

Alisema kwamba alilazimika kumtafuta baba mtoto wake kwa kuwa mumewe hakuwa akisaidia katika malezi yake.

"Baba mtoto alianza kusaidia mtoto. Hapo ndipo alianza kutoniamini. Mtoto wangu nilimuacha kwa mama," alisema.

Aliongeza, "Yeye anasaidia watoto wake lakini hasaidii wangu. Nilitafuta baba mtoto wangu ili amsaidie. Alianza kuuliza mbona namtafuta."

Faith alifichua kwamba ingawa bado anaishi pamoja na mumewe, kwa sasa hakuna amani kabisa pale nyumbani na hata hawazungumzi.

Boniface alipopigiwa simu hata hivyo alidai kwamba hakuna tatizo lolote nyumbani na kusema kuwa wako sawa.

"Hakuna tatizo, tuko sawa," alisema.

Faith alimwambia, "Uache kunishuku kwa sababu kwa maisha yangu nilikuchagua wewe na siwezi kupenda mwingine."

Alimhakikishia Boniface kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kumwambia watasuluhisha yote jioni atakapotoka kazini.

Ni jambo la kufurahisha kuona wawili hao waliweza kupatana mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa  Boniface kama ilivyofichuliwa na Faith.