"Alisema atanipeleka Illuminati!" Mwanadada afunguka alivyotishiwa na mpenziwe aliyemtunga mimba

Flora alidai kuwa hakuwahi kuolewa na Henry ila walikuwa marafiki tu.

Muhtasari

•Henry alisema mambo yalianza kuharibika wakati ambapo mke wake aliondoka nyumbani na kuenda jijini Nairobi kwa ajili ya kazi.

•Henry alifichua kuwa baadaye Flora alianza kumtafuta baada ya kujifungua akitaka wasaidiane kulea mtoto wao msichana.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi, kitengo cha Patanisho, jamaa aliyejitambulisha kama Henry Osako almaarufu Nelson Mandela alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Flora waliyekosana naye Desemba 2021.

Henry alisema kwamba alikuwa kwenye ndoa na Flora kwa takriban miaka miwili hadi Desemba 2022 wakati mkewe aliondoka nyumbani na kuenda jijini Nairobi kwa ajili ya kazi, na hapo ndipo mambo yalipoharibika.

"Sikujua lolote, aliniambia amepata kazi Nairobi. Akiwa Nairobi aliniambia ako na mimba na anataka anataka kutoa, nikamwambia asitoe," Henry alisimulia.

Aliongeza, "Ilifika wakati akaanza kunitusi usiku na mchana. Kuuliza shemeji yangu alisema kwamba mimba ndiyo ilikuwa ikifanya anitusi."

Henry alifichua kuwa baadaye Flora alianza kumtafuta baada ya kujifungua akitaka wasaidiane kulea mtoto wao msichana.

"Alipojifungua alianza kunirudia, nikaanza maringo kidogo," alisema.

Henry alisema Flora amemvutia licha ya kumzidi umri kwa  miaka minne na alikuwa amekubali kufunga ndoa naye.

"Ata nikikula chakula haiendi kwa tumbo, ni mawazo tu nikimfikiria. Chakula kinaenda tu kwa kucha na choo," alisema.

Bi Flora alipopigiwa simu, Henry alichukua fursa kumsihi amwambie ukweli huku akimwambia kwamba ameshindwa kuvumilia upweke.

Flora hata hivyo alikabiliana na mzazi huyo mwenzake kwa maneno makali na kufichua ukweli fulani kumhusu ambao hakuwa amefichua.

"Hata haitwi Mandela, anaitwa Henry Osako. Tulikuwa nyumbani Desemba akanipea mimba. Hajawahi kushughulikia mtoto," alisema.

Alifichua kwamba mpenzi huyo wake wa zamani alianza kumtishia baada ya kumwambia kuwa yuko na mimba yake.

"Nilienda Nairobi nikapata niko na mimba yake. Kumwambia akaanza mambo.Alisema atanipeleka Illuminati," alisema.

Flora pia alidai kuwa hakuwahi kuolewa na Henry na akafichua kwamba walikuwa marafiki tu ambao walipata mtoto pamoja.

"Hiyo namba udelete na usinitafute. Kama huwezi kusaidia mtoto usinitafute.Hata unajua kwetu? kweli?" Flora alimwambia Henry.

Henry alijaribu sana kumbembeleza Flora ampatie nafasi ya mwisho ila mwanadada huyo alionekana kafanya maamuzi yake kabisa. Alimwagiza aendelee na maisha yake na kumuacha yeye akuwe.

"Mimi siko tayari kumuacha. Ata nizikwe sitawahi kumsahau," Henry alidai.