Patanisho: Jamaa ataka kupatanishwa na ex wake baada ya kumtumia maua WhatsApp

Patrick alitengana na mke wake mwaka wa 2012.

Muhtasari

•Patrick alisema ndoa yake na Jeddy ya miaka miwili ilisambaratika baada ya familia zao kutofautiana kuhusu wao kuoana.

•Jeddy alipopigiwa simu alikana kumjua Patrick na kukata simu mara moja.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO
 

Katika kitengo cha Patanisho, Patrick Omondi ,32, kutoka Kongowea alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mke wake Jeddy Kasoya ambaye alikosana naye takriban miaka kumi na miwili iliyopita.

Patrick alisema ndoa yake na Jeddy ya miaka miwili ilisambaratika baada ya familia zao kutofautiana kuhusu wao kuoana.

"Nilipatana na yeye akiwa shuleni. Akapata mimba. Wakati huo bado nilikuwa kwa wazazi wangu. Wakati tulitaka kukaa pamoja, familia zetu hazikuweza kupatana. Wazazi wangu walisema msichana huyo ameniharibia masomo," Patrick alisimulia.

Patrick alifichua kwamba alikuwa katika kidato cha pili wakati alipomtunga ujauzito Bi Jeddy ambaye alikuwa katika chuo kikuu.

"Baadaye tulikubaliana kukaa pamoja. Tulikuja kukosana sisi wawili, akarudi kwao na mtoto,

Aliendelea, "Nilitumia hasira nikaenda kuchukua mtoto wangu nikamleta kwetu. Mtoto alikuwa na miezi tisa hivi... Imepita miaka kama tatu hatujaonana.Tumekuwa tukizungumza kwa simu. Alisema nionyeshe kwa vitendo kwamba nampenda. Alitaka nimsaidie mtoto lakini singeweza kwa sababu alikuwa kwao,"

Patrick alisema alitiwa moyo kwamba mahusiano yao huenda yakarejea baada ya mzazi huyo mwenzake kumtumia maua mnamo siku ya Wapendanao.

"Alinitumia maua kwa WhatApp nikaona nijaribu Patanisho. Nilikuwa nimejaribu kuoa lakini akili yangu yote iko kwa huyo wa kwanza,"

Jeddy alipopigiwa simu alikana kumjua Patrick na kukata simu mara moja.

"Simjui!" alisema kabla ya kukata simu.

Patrick hata hivyo alisisitiza kuwa sauti iliyopokea simu ni ya mzazi mwenzake na kubainisha kuwa anamfahamu vizuri.

"Yeye ni mafia kivyake," alisema.

Aidha alifichua kuwa walihusika katika mzozo mdogo baada ya Jeddy kumtumia maua kwenye mtandao wa WhatsApp.

"Baada ya yeye kunitumia maua ya Valentines aliniflash. Nilichukua kama dakika 30 nikampigia simu nikamwambia kwamba niko bize nitampigia baadaye. Nilipopiga simu akawa yuko bize. Baadaye Alinitumia meseji akaniambia wakati alinitaka kuongea na mimi nilijifanya niko bize, kwamba pia yeye ni bize,"

Patrick alisema mara ya mwisho kuonana na mke huyo wake wa zamani ilikuwa takriban miaka miwili iliyopita.

Aidha alifichua kwamba alitengana na Bi Jedy takriban miaka kumi na moja iliyopita baada ya kujaliwa mtoto mwaka wa 2008.

"Mtoto mi humuona tu kwa simu. Tulibarikiwa na watoto wawili ijapokuwa mmoja alifariki. Kwa ufupi, tulikosana 2012.Mtoto tulipata 2008," alisema.

Wakati patanisho ikiendelea, Jeddy alimtumia Patrick ujumbe na akimwambia aache ujinga.

Patrick aliendelea kuchukua fursa kumsihi mke huyo wake wa zamani warudiane.

"Jedyy mimi bado nakupenda. Upendo wetu wa kwanza wakati tulipata watoto wawili bado upo. Sina mengi ila bado nakupenda," alimwambia hewani.

Je, una ushauri gani kwa Patrick?