Patanisho: Jamaa agundua mkewe amemzidi umri kwa miaka 5 baada ya miaka 3 ya ndoa

Onyango alidai kwamba awali mkewe alidanganya umri wake.

Muhtasari

•Wilson alisema kwamba alikosana na mkewe mwezi Januari kufuatia ugomvi wa kinyumbani uliotimbuka baada ya kazi yake kusimama.

•Alilalamika kuwa ukweli kwamba Mildred ni mkubwa kuliko yeye umemfanya amtende kama mtoto wakati fulani.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Wilson Onyango,  24, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Mildred Opanda ,31.

Wilson alisema kwamba alikosana na mkewe mwezi Januari kufuatia ugomvi wa kinyumbani ambao ulitimbuka baada ya kazi yake kusimama na kumfanya ashindwe kukidhi mahitaji ya familia yake. 

"Mimi ni hustler wa bodaboda. Nilikuwa nafanya kazi ya boda alafu baadae nikawa na shida ya mkono nikakaa nyumbani kwa takriban mwezi moja. Pesa zilikosekana kwa nyumba alafu baadaye ikawa vita," alisema.

"Nilifura mkono na unajua huwezi kuendesha pikipiki ukiwa umefura," alisema.

Wilson alifichua kwamba ndoa yao imedumu kwa miaka mitatu na tayari wamebarikiwa na mtoto mmoja pamoja.

Alidai kwamba awali Bi Mildred  alidanganya umri wake na ilimchukua miaka 3 kugundua, jambo ambalo hakufurahia.

"Alikuwa ameficha miaka.  Baada ya miaka tatu nikajua ameniacha kwa zaidi ya miaka mitano. Tulikuwa tunaishi vizuri lakini wakati mwingine anakuwa amebadilika," Wilson alisema.

Alilalamika kuwa ukweli kwamba Mildred ni mkubwa kuliko yeye umemfanya amtende kama mtoto wakati fulani.

"Uhusiano wetu ni kama probox na pikipiki. Kwa vile amenizidi umri wakati mwingine inakuwa anaona mimi ni kama mtoto. Anaona ako juu yangu. Hatuelewani kabisa. Hata leo asubuhi tumepitana tu," alisema.

Pia alifichua kwamba mkewe amekataa kufanya kazi yoyote ya kuleta pesa nyumbani na kwa hivyo ameendelea kutafutia familia licha ya kuwa na shida ya mkono.

"Hapo awali alikuwa anataja mambo ya kutoroka lakini nikamzuia. Wakatu moja alishika panga mpaka akanikata mkono,

Juhudi za kumpatanisha Wilson na mkewe hata hivyo hazikufua dafu kwani Midred hakushika simu alipopigiwa.