Diana: Nilitoroka nikamuachia mke mwenza mtoto wangu mchanga, nataka kurudi

Diana aliolewa kama mke wa pili kwa sababu mke wa kwanza hakupata mtoto. Aliona ubaguzi na kutoroka akimuachia mtoto wake.

Muhtasari

• Diana aliona mke wa kwanza anabagua watoto wake, akipenda yule wa pili aliyezaa na mume wake huku akimtelekeza mtoto aliyekuja naye.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mwanadada kwa jina Diana Auma alipeleka ombi la kutaka kupatanishwa na mke mwenza baada ya kutoroka nyumbani na kumuachia mtoto wake mdogo.

Kulingana na Diana, aliolewa kama mke wa pili baada ya mke wa kwanza kutofanikiwa kupata mtoto.

Wakati anaolewa, alikuwa na mtoto mmoja na wakazaa mwingine wa pili na bwana yake ambaye walikuwa wanaishi naye mjini huku mke wa kwanza akiishi peke yake kwa mume wao kijijini.

Baada ya kujifungua, mume wake alimsihi kurudi nyumbani ili kuishi na mke wa kwanza katika kile alimwambia kwanza kazi imepungua na kuishi naye mjini kungekuwa na gharama kubwa.

Diana alikubaliana na ombi la mume wake na kufunga safari kwenda kwa kina mume wake kijijini akiwa peke yake. Nyumbani alipokelewa kwa mbwembwe na mke wa kwanza akiwa na watoto wake wawili.

“Nilienda peke yangu mpaka nyumbani na tulikaa alinipokea vizuri alikuwa ameshaambiwa ninakuja. Alikuwa anajua tunakaa na mume wake mjini. Mume akakuja na kidogo akarudi….bwana alikuwa amenioa na mtoto mmoja na nikazaa mwingine naye….” Diana alielezea.

Tatizo lilianza pale ambapo Diana alianza kuhisi kama mke mwenza kwa jina Millicent alikuwa anaonesha ubaguzi kwa watoto – alianza kumpenda mtoto mdogo ambaye mke mdogo alizaa na mume wao huku akimbeza mtoto mkubwa wa Diana ambaye aliolewa naye.

“Ubaguzi ulipoanza nikaona hata bwana anatuma pesa ya chakula mke mkubwa hanipi… nikapigia mume simu nikamwambia kile kinachoendelea na yeye akaniambia kama mke mwenza anapenda mtoto nimezaa na yeye na mimi nipende mtoto wangu,” alisema.

Diana aliamua kufunga safari na kuondoka kwenda kwao akiwa na mtoto aliyeolewa naye huku mtoto mdogo akimuacha mikononi mwa mke mkubwa.

Kwa maneno yake, alisema kwamba alikuwa amemkosa mtoto wake na alitaka kurudi ili kumlea mtoto wake pia.

Mke mkubwa kwa upande wake alisema kwamba Diana alimtuhumu kwamba alikuwa anamweka njaa na kumtaka kuomba msamaha mume wao na wala si yeye.

“Yeye alitoka akachukua vitu vyangu akaenda navyo, akasema kuwa nilikuwa natumiwa pesa simpi namshindisha njaa, mpaka pesa yangu aliondoka nayo hata nikashindwa kwenda chama. Azungumze na mzee ajengewe nyumba yake. Mimi naogopa anaweza rudi na aondoke na vitu vyangu…” Millicent alisema.