Patanisho: "Wakati akivaa vizuri, naona kuna mtu atakula kitu," Jamaa akiri kutomuamini mkewe

Elvis alisema kuwa tayari amelipa mahari ya shilingi elfu kumi kwa mamake Debra.

Muhtasari

•Elvis alisema kwamba ndoa yake ya miaka miwili ilivunjika baada ya kuvuragana na mke wake kwa kutoaminiana kwenye ndoa.

•Debra alipopigiwa simu alithibitisha kuwa mzazi huyo mwenzake alikosa kumwamini wakati walipokuwa kwenye ndoa.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Elvis Omondi ,25, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Daisy Debra Atieno ,24, ambaye alikosana naye siku kadhaa zilizopita.

Elvis alisema kwamba ndoa yake ya miaka miwili ilivunjika baada ya kuvuragana na mke wake kwa kutoaminiana kwenye ndoa.

"Ilifika mahali tukaanza kutoamonina kwa ndoa, mtu akitoka nyumbani mwingine anaona kama anaenda nje ya ndoa. Mimi ndio sikuwa namwamini. Wakati akivaa vizuri na kutoka naona kuna mtu atakula kitu," alisema.

Elvis alisema mkewe aligura ghafla bila hata kumpatia tahadhari.

"Hiyo siku tulikuwa tumeongea. Wakati nilienda kununua Omena kwa soko, kurudi nilipata hayuko. Huwa tunaongea lakini vile anaongea sioni kama ako na mood poa," alisema.

Aliongeza, "Tuliongea na kaka yake akaniambia ataongea na yeye. Huwa ananiambia msichana anasema atulie kidogo."

Alieleza kuwa tayari amelipa mahari ya shilingi elfu kumi kwa mamake Debra.

Debra alipopigiwa simu alithibitisha kuwa mzazi huyo mwenzake alikosa kumwamini wakati walipokuwa kwenye ndoa.

"Nliliishi na huyo jamaa na kuna vile alikuwa anasema mimi ni malaya. Hata nikienda kanisa anasema nimeenda nje ya ndoa. Wazazi wake pia walikuwa wananipigia kelele. Sidhani kama nitarudi," alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alidokeza kwamba hayuko tayari kurudi nyumbani kwa kina Elvis kufuatia matatizo aliyopitia huko.

"Nilikusamehe lakini kwenu naona ni balaa. Nimeamua hivyo. Sijakataa tusionane lakini kwenu sirudi. Tunaweza kukutana," alisema.

Huku akijitetea, Elvis alisema, "Najua nilikukosea sana. Nilikuja nikakaa chini nikaona mimi ndio mbaya."

Debra alisisitiza kuwa amechoka kwa kuwa tayari amempatia mzazi huyo mwenzake nafasi za kutosha za kujirekebisha. Hata hivyo, alidokeza kuwa kuna uwezekano wa yeye kurudiana na Elvis iwapo watahama na atampatia uhuru wa kufanya kazi.

"Elvis, mimi nakupenda lakini kurudi kwenu ni balaa," alimwambia mumewe.

Elvis alisema, "Debra, mimi nakupenda sana. Ata kama hayo yote yamefanyika, mimi bado nakupenda. Nisamehe tu na turudiane, itakuwa sawa."