Patanisho: Mlinzi aachwa na mkewe usiku baada ya kupigiwa simu na mpango wa kando

Brian alisema ameshindwa kuepuka majaribio ya kuwa na mpango wa kando.

Muhtasari

•Brian alieleza kwamba mkewe aligura ndoa yao ya mwaka mmoja baada ya kumpata akizungumza na mpango wa kando.

•Brian alikiri anampenda mkewe sana na kudai kwamba amekuwa akijaribu kuepuka majaribio ya kuwa na mpango wa kando lakini ameshindwa.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Brian Wanjala (27) alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Monica (26) ambaye alimuacha siku chache zilizopita.

Brian alieleza kwamba mkewe aligura ndoa yao ya mwaka mmoja baada ya kumpata akizungumza na mpango wa kando.

"Siku ya Jumapili tulikuwa tumekaa na bibi yangu tunaongea vizuri. Nilikuwa na mpango wa kando akanipigia simu. Nilikuwa nimefuta namba kwa hivyo sikujua ni nani anapiga. Nilishika simu akaniuliza niko wapi na kudai tuonane. Nilikata simu mara moja kwa sababu bibi yangu alikuwa hapo," Brian alisema.

Aliweka wazi kuwa hakuna mzozo uliozuka baina yake na mkewe baada ya matukio hayo. Hata hivyo, Bi Monica alitoroka nyumbani baadaye wakati Brian akiwa kazini.

"Alinipeleka maji kwa bafu, akapika vizuri, tukakula nikaenda kazini. Huwa nafanya kazi ya usiku, mimi ni soldier. Niliporudi asubuhi sikumpata," alisema.

Brian alikiri anampenda mkewe sana na kudai kwamba amekuwa akijaribu kuepuka majaribio ya kuwa na mpango wa kando lakini ameshindwa.

"Si mtu wa kusema ukweli.Tuko kwa mahusiano lakini sio mtu wa kusema ukweli. Huwa anasema nimsamehe lakini anarudia," alisema.

Aliongeza, "Namshuku ako na mpango wa kando na nikifuatilia anakataa kusema ukweli. Mimi sina shida na yeye."

Monica aliweka wazi kwamba bado yuko kwenye ndoa na Brian na kumuomba awe msema kweli.

Brian hata hivyo alikata simu wakati mkewe akizungumza na hivyo hakukuwa na hitimisho ya Patanisho. Gidi hata hivyo alimshauri Monica kushiriki mazungumzo na mumewe ili waweze kutatua mzozo wao.