"Naumia mama, natamani tu kuona sura yako" Mwanadada alia kwa uchungu baada ya kutengwa na mamake

Joyline alisema mama yake alimuonya asiwahi kuenda nyumbani ama kumpigia simu.

Muhtasari

•Joyline alifichua kwamba uhusiano wake na mamake uliathirika baada ya yeye kuacha kazi ambayo mzazi huyo wake alimuwekea alipomaliza masomo ya shule ya upili na kuenda kuolewa.

• "Mume wangu aliniambia kama mamangu hataki kumuona kuna haja gani ya kukaa na mimi. Tuliachana na yeye," Joyline alisema.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Joyline Muhonja ,23, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake mzazi ambaye alikosana naye takriban miaka minne iliyopita. 

Joyline alifichua kuwa uhusiano wake na mamake, Priscilla Mulira, uliathirika mwaka wa 2019 baada ya yeye kuacha kazi ambayo mzazi huyo wake alimuwekea alipomaliza masomo ya shule ya upili na kuenda kuolewa.

"Ilikuwa mwaka wa 2019, nilikuwa nimemaliza kidato cha nne mama akaniambia anitafutie kazi. Aliniuliza kama ninaweza kufanya kazi ya kushona nguo badala ya kukaa tu kwa nyumba. Baadaye alinifungulia kazi alafu nikiwa hapo nikapata na mtu nikaolewa. Wakati ambapo nilimwambia nimeolewa aliniuliza nimeacha vitu vya kazi wapi nikamwambia niliacha kwa ile duka alinifungulia," Joyline alisimulia.

Joyline alifichua kwamba tangu wakati huo, mzazi huyo wake amekatiza mawasiliano naye na hata amekataa kabisa kuonana naye.

"Ata hajui nilizaa watoto wa aina hiyo. Nilipata watoto wawili. Hataki ata kumuona mume wangu," alisema.

Aliongeza, "Mume wangu aliniambia kama mamangu hataki kumuona kuna haja gani ya kukaa na mimi. Tuliachana na yeye."

Joyline alisema mama yake alimuonya asiwahi kuenda nyumbani ama hata kumpigia simu.

Aidha, alifichua kwamba juhudi zake za kuomba msamaha na kupatanishwa na mzazi huyo wake hazijafanikiwa kuzaa matunda.

"Najua aligharamia pesa nyingi kununua sherahani na vifaa vya kushuka. Hakutaka niende kuolewa haraka. Natamani hata nimuone siku moja. Naumia kweli. Baba yuko, nikiongea naye huwa ananiambia niongee na mama.  Dada zangu nilijaribu kuongea nao wakasema mama bado amekasirika. Waliniambia alisema hataki kusikia stori zangu kabisa. Naogopa kuenda kwa sababu aliniambia nisikanyange huko," alisema.

Juhudi za Gidi kumpatanisha Joyline na mzazi huyo wake hazikufua dafu kwani Bi. Priscilla alikuwa amezima simu yake.

Joyline alipopewa nafasi ya kutuma ujumbe kwa mamake hewani alisema, " Mama najua nilifanya makosa. Saa hii najuta, sina furaha kabisa. Naomba urudishe roho yako chini. Natamani tu kuona sura yako. Hata mwanaume nilikuwa naishi naye tulikosana. Naumia mama, naomba unisamehe."