"Siamini ameoa" Mwanadada aliyeacha jamaa miaka 6 iliyopita ataka kumrudia na mtoto mwingine

Mueni alikiri baada ya kugura ndoa hiyo alijitosa kwenye mahusiano mengine na kupata mtoto wa pili.

Muhtasari

•Mueni alisema kwamba alitengena na Kioko takriban miaka mitano iliyopita kutoafutiana na kutoelewana katika ndoa ya miaka 6.

•Mueni alisisitiza mume huyo wake wa zamani hajasonga mbele na maisha yake kwani kulingana naye, ni jambo lisilowezekana.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mwanadada Faith Mueni ,29,kutoka Machakos alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na aliyekuwa mume wake Paul Kioko, 30.

Mueni alisema kwamba alitengena na Kioko takriban miaka mitano iliyopita kutoafutiana na kutoelewana katika ndoa ya miaka 6. Wawili hao walikuwa wamebarikiwa na mtoto mmoja pamoja kabla ya kutengana.

Mueni alikiri kuwa baada ya kugura ndoa hiyo alijitosa kwenye mahusiano mengine na kupata mtoto wa pili mwaka jana.

"Hatukuwa tunapatana. Hatukuwa tunaelewana. Tuliachana 2018. Nilienda zangu nikaendelea na maisha lakini mwaka jana nilipata mtoto. Kila mtu alikodisha nyumba yake pekee yake. Sijui alihamia pande gani," alisema.

Mueni alisema amekuwa akizungumza na mzazi huyo mwenzake na amekuwa akimfahamisha kwamba ameoa ila haamini.

"Ananiambia ashaoa lakini sijaamini. Nataka kujua kama atanikubali. Kama ameoa ni sawa. Sioni kama ni kweli ameoa," alisema.

Mama huyo wa watoto wawili alisema mpenzi ambaye alipata mtoto wa pili naye alimuacha pindi baada ya kujifungua  na hata hajakuwa akimshughulikia mtoto wao.

Gidi hakufanikiwa kumpata Kioko kwenye simu licha ya kufanya majaribio kadhaa. 

Mueni alisisitiza mume huyo wake wa zamani hajasonga mbele na maisha yake kwani kulingana naye, ni jambo lisilowezekana.

"Alikuwa ananiambia kama ni mtoto wake nimpatie atalea na bibi yake. Lakini mimi siamini ameoa. Ni vigumu kwake kuoa vile namjua. Sio eti hawezi kupata mwingine lakini najua ni uwongo," alisema.

Alipopewa fursa ya kuzungumza naye hewani, alisema, "Nampenda kama mume wangu. Nataka turudiane. Turudi vile tulikuwa tunakaa kitambo."

Maoni yako ni yapi kuhusu Patanisho ya leo?